Aya 91 -100: Mjuzi Wa Ghaibu Na Yaliyo Wazi
Mwenyezi Mungu hakujifanyia mwana.
Hana mshirika wala mtoto. Lau angelikuwa na mtoto angelifanana naye. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hana mfano na chochote.
Wala hanaye mungu mwingine. Ingelikuwa hivyo basi kila Mungu angelichukua alivyoviumba.
Lau ulimwengu ungelikuwa na waumbaji wawili, basi kila mmoja angelihusika na sehemu fulani ya ulimwengu; angelikuwa na mipaka yake nidhamu yake na mambo yake yasiyoafikiana na sehemu nyingine. Kwa kuwa nidhamu ya ulimwengu ni moja na mambo yake ni mamoja, basi muumba wake ni mmoja.
Na baadhi yao wangeliwashinda wengine.
Vile vile lau waumbaji wangelikuwa wengi, hilo lingesababisha kila mmoja kuwa mshindi juu ya mwingine kwa wakati mmoja. Kwa sababu sifa ya Mungu ni kuwa juu ya kila kitu. Yaani kama waungu wangelikuwa wengi basi kungelikuwa na mashindano; kama inavyokuwa kwa watawala. Na huo ndio ufisadi hasa.
Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu kuwa ana mwana au washirika. Umetangulia ufafanuzi wake katika Juz. 5 (4:50).
Mjuzi wa ghaibu na dhahiri.
Makusudio ya ghaibu ni yale ambayo viumbe hawawezi kuyajua. Na ya dhahiri ni yale ambayo viumbe wanaweza kuyajua. Kwa hakika ilivyo hasa ni kuwa ugawanyo huu unafaa kwa viumbe, sio kwa muumba. Kwa sababu kwake yeye vitu vyote ni sawa kiujuzi na kiuwezo.
Ametukuka juu ya hayo wanayomshirikisha nayo, kutokana na kutowatambua hao washirika. Ikiwa kitu hakitambui muumba maana yake ni kuwa hakiko.
Sema, Mola wangu! Ukinionyesha waliyoahidiwa, Mola wangu usinijaalie katika watu madhalimu.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake aombe dua ya kuokoka na ghadhabu na adhabu yake itakayowapata wenye hatia na madhalimu, pamoja na kujua kuwa Mtume (s.a.w.) yuko katika amani na salama. Lakini lengo la dua hii ni kuhadharisha watu wa shirk na madhalimu. Mara nyingi waongozaji wanatumia mfumo huu kuonyesha kupingana na yule aliyeghadhibikiwa na Mwenyezi Mungu.
Na hakika sisi ni wenye kuweza kukuonyesha tuliyowaahidi.
Mtume (s.a.w.) aliwaonya makuraishi kwa adhabu kama watamkadhibisha na kupinga utume wake, wakacheka na wakafanya masikhara; ndio Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake Mtukufu kuwa usihuzunike! Sisi tunaweza kukuonyesha maangamizi, lakini tunaahirisha kwa hekima na maslahi yako na ya Uislamu.
Pengine hekima hiyo ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua kuwa baadhi yao au baadhi ya watoto wao watamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wawe ni nguvu ya kuusaidia Uislamu na waislamu; kama ilivyotokea hivyo hasa.
Kukinga Maovu Kwa Mema Zaidi
Kinga maovu kwa yaliyo mema zaidi. Sisi tunayajua wanyoyasifia.
Ni nini kukinga kwa kutenda yaliyo mema zaidi? Je, ni kuvumilia maudhi na kumnyamazia anayekuudhi, kama wasemavyo wafasiri wengi?
Kinga inatofautiana kulingana na hali. Inaweza ikawa kutumia nguvu dhidi ya adui ndio kukinga kwa yaliyo mema zaidi. Hapo ni ikiwa aliyechokozwa ana uwezo na ikawa kumnyamazia mchokozi kunamtia mori wa kufanya uovu na uadui. Imam Ali (a.s.) anasema: "Kutekeleza ahadi kwa wasio na ahadi ni kuvunja ahadi na kuvunja ahadi kwa wasio na ahadi ni kutekeleza ahadi"
Na inawezekana kuwa kumnyamzia mchokozi ni kinga ya kufanya mema zaidi, ikiwa huko kumnyamazia kutamfanya ajute na atubie au ikiwa aliyechokozwa hana nguvu za kutosha kumzuia mchokozi. Kwani hapo itakuwa ni kujiingiza katika mambo ambayo hayana mwisho mzuri.
Kwa ajili hii Mtume alivumilia maudhi akiwa Makka kwa kutokuwa na uwezo, lakini aliwatia adabu wachokozi baada ya kuhamia Madina na kupata nguvu.
Na sema, Mola wangu! Najikinga kwako na wasiwasi wa shetani, na ninajilinda kwako wasinikaribie,
Ni wazi kuwa shetani hana uwezo wowote kwa Mitume, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika waja wangu huna mamlaka nao isipokuwa wale wapotofu waliokufuata." Juz. 14 (15:42).
Unaweza kuuliza: Ikiwa shetani hana uwezo wowote kwa Mitume, basi kwa nini Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kujikinga nao?
Jibu: Kujikinga na kitu hakumaanishi kutowezekana kutokea kwake. Kwani maasumu wanajikinga na ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu zaidi kuliko wengine, pamoja na kuwa wao wako katika amani na salama. Kwa maneno mengine ni kuwa kumkimbilia Mwenyezi Mungu ni dua, na dua inafaa kuwa ni kinga ya uovu na balaa hata kama haiko. Huko nyuma tumeashiria kwamba wacha Mungu mara nyingi wanaonyesha uovu katika dua zao kwa unyenyekevu.
Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu nirud- ishe ili nitende mema badala ya yale niliyoyaacha.
Wakati alipokuwa na fursa ya kufanya matendo mema aliipoteza na kuipuuza. Baada ya kumfikia mauti ndio anataka kurudia uhai ili afanye amali njema. Hivi ndivyo alivyo kila mzembe, anaipoteza nafasi anapokuwa nayo na inapomtoka huanza kuijutia.
Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu.
Hakuna kurejea kabisa! Hata kama mzembe huyu atakubaliwa kurudi mara ya pili atarudia uasi wake. Ama kusema kwake 'ili nitende mema' ni maneno matupu tu yasiyokuwa na maana wala utekelezaji. Hilo amelifafanua Mwenyezi Mungu aliposema: "Na kama wangelirudishwa bila shaka wangeliyarudia yale waliyokatazwa na hakika wao ni waongo" Juz.7 (6:28).
Na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa.
Nyuma yao ni kinaya cha kila upande. Maana ni kuwa wao wametaka kurejea duniani na baina yao na maisha ya dunia kuna kizuizi kitaka-chobaki mpaka siku ya kiyama. Hapo ndio kitaondoka kizuizi, lakini itakuwa ni wakati wa viumbe kusimama mbele ya Mola wao kwa ajili ya hisabu na malipo.
فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ فَلَا أَنْسَابَ بَيْنَهُمْ يَوْمَئِذٍ وَلَا يَتَسَاءَلُونَ {101}
فَمَنْ ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {102}
وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنْفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ {103}
تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ {104}
أَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنْتُمْ بِهَا تُكَذِّبُونَ {105}
قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ {106}
رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْهَا فَإِنْ عُدْنَا فَإِنَّا ظَالِمُونَ {107}
قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ {108}
إِنَّهُ كَانَ فَرِيقٌ مِنْ عِبَادِي يَقُولُونَ رَبَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنْتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ {109}
فَاتَّخَذْتُمُوهُمْ سِخْرِيًّا حَتَّىٰ أَنْسَوْكُمْ ذِكْرِي وَكُنْتُمْ مِنْهُمْ تَضْحَكُونَ {110}
إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ {111}