read

Aya 26 – 29: Mambo Ya Uhabithi Ni Ya Mahabithi

Maana

Mambo ya uhabithi ni ya mahabithi na mahabithi ni wa mambo ya uhabithi. Na mema ni ya walio wema na walio wema ni wa mema.

Neno uhabithi limefasiriwa kutoka na neno la kiarabu Khabith lenye maana ya uovu na ubaya katika kila jambo, ikiwemo ubaya katika itikadi, nia, sifa, kauli na vitendo vya aina mbali mbali, wala hauhusiki na zina.

Na neno wema limefasiriwa kutokana na neno Twayyib lenye maana ya uzuri katika kila jambo.

Qur'an imelitumia neno uhabithi katika ubaya wa ardhi, mali, maneno na vyakula vilivyoharamu na kila anayestahiki machukivu na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu katika majini na watu.

Jamaa katika wafasiri wamesema kuwa makusudio ya neno Khabithat ni wanawake mahabithi na Khabithun ni wanaume mahabith. Vilevile katika wema. Kauli hii haiafikiani na hali halisi ilivyo.

Tumewaona wanawake mahabithi wakiolewa na wanume wema na wanawake wema wakiolewa na wanume mahabithi. Bali hata haiafikiani na Qur'an; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

"Mwenyezi Mungu amewapigia mfano waliokufuru - mke wa Nuh na mke wa Lut walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu, lakini wakakhini … Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walioaminimke wa Firauni, aliposema: Mola wangu nijengee kwako nyumba Peponi na uniokoe na Firauni na vitendo vyake" (66:11). Inajulikana kwamba Nuh na Lut walikuwa Manabii, maasumu na Firauni ndiye yule aliyesema: "Mimi ndiye Mola wenu mkuu."

Tuonavyo sisi ni kuwa neno Khabithat lina maana ya mambo ya uhabithi, na neno khabithun lina maana ya walio mahabithi wote wanaume na wanawake. Limekuja kwa dhamiri ya kiume kwa kuchanganya wote. Vile vile Twayyibat na Twayyibun.

Kwa hiyo maana yatakuwa, kauli na vitendo vya uhabithi vinatokana na yule aliye habithi katika wanaume na wanawake. Na kauli na vitendo vyema vinatokana na yule aliye mwema; kama alivyosema mshairi: "Kila kilicho ndani ya chombo kitaiva."

Hao wameepushwa na wanayoyasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.

Hao ni ishara ya walio wema; wanosema ni wale mahabithi. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawaneemaesha na maghufira na pepo hao walioepushwa.

Enyi ambao mmeamini! Msiingie nyumba zisizo nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee salaam wenyewe. Hayo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka.

Mpaka muombe ruhusa ni amri ya kubisha hodi kabla ya kuingia; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya 59 ya Sura hii tuliyo nayo: "Na watoto wanapofikia kubaleghe basi nawatake ruhusa."

Kila anayetaka kuingia nyumba ya mwingine ni lazima aombe idhini kwa mwenyewe kwanza. Kwa sababu kuingia ni kutumia mali ya mwenyewe, ambayo haiwezi kuwa halali ila kwa ruhusa yake. Kuanzia hapa ndio mafaqihi wakasema kuwa kuomba ruhusa ni wajibu na salaam ni Sunna. Inatosha kuwa ni kuomba ruhusa kwa jambo lolote lile; kama vile kugonga mlango, kusema hodi! Au wenyewe humo! Baada ya kupewa idhii ndio aiingie atoe salaam!

Na msipomkuta yoyote humo basi msiingie mpaka mruhusiwe.

Unaweza kuuliza hapa, ikiwa nyumbani hakuna mtu, ni nani atakayetoa ruhusa?

Sheikh Maraghi amejibu kuwa makusudio ni ikiwa hakuna anayeweza kutoa ruhusa; kama mtoto mdogo au mtumishi. Jawabu lilo na nguvu ni ikiwa nyumba haina mtu, basi hairuhusiwi kuingia mpaka amuone mwenyewe kwanza na ampe idhini; kwa mfano kumwambia nenda nyumbani kwangu ukaniletee kitu fulani au tangulia nyumbani kwangu nami naja.

Na mkiambiwa rudini, basi rudini. Hivyo ni usafi zaidi kwenu.

Wala msing'ang'anie kutaka kuingia na msiwe na chuki nyoyoni kwa mwenye nyumba mchukue uzuri tu na kusema ana udhuru wa kisharia. Angalia kifungu cha 'Kuchukulia usahihi' katika Juz.1 (2:83).

Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.

Hii ni hadhari na kiaga kwa yule anayemshtumu na kumsema ambaye hakumpa idhini ya kuingia nyumbani kwake.

Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisizokaliwa ambazo ndani yake mna bidhaa zenu.

Makusudio ya nyumba hizi ni zile sehemu za watu wengi, kama vile mahoteli na maduka.
Kwa hiyo ambaye ana bidhaa zake hotelini au dukani, basi anaweza kuingia na kuchukua bidhaa zake bila ya kmuomba ruhusa mwenyewe, kwa sababu amekwisha fungua mlango kwa wote. Pia hakuna siri kwa mwenye hoteli kwa hilo.

Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyadhirisha na mnayoyaficha.

Hii inaashiria kuwa si halali kwa mtu kuingia nyumba ya mwingine kwa kusudia kufanya khiyana na kuwadhuru wenyewe, na kwamba mwenye kukusudia hivyo, basi Mwenyezi Mungu anajua malengo yake na atamwadhibu nayo.

قُلْ لِلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ {30}

Na waambie waumini wanaume wainamishe katika macho yao na wazilinde tupu zao. Hilo ni usafi zaidi kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za wanayoyafanya.

وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِنْ زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {31}

Na waambie waumini wanawake wainamishe katika macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao, isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasidhihirishe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au ndugu zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio, au watoto wadogo ambao hawajajua uchi wa wanawake. Wala wasipige miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubieni kwa Mwenyezi Mungu nyote enyi waumini ili mpate kufanikiwa.