read

Kitika Hema La Rustam

Mtungaji:
Ustadh Shahid Murtada Mutahhari

Mtarjumi:
S Muhammad Ridha Shushtary

Mchapishaji:
Islamic Thought Foundation
No. 5. Takhti Sq., Shahid Beheshti Ave.
PO Box 14155-3899
Tehran, Iran

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Rustam Farakhzad akiongoza jeshi lililojiandaa kikamilifu kwa silaha na zana za kivita, aIiingia katika eneo la Qadisiyya ili kuwaangamiza Waislamu ambao kabla yake waliwashinda Wairani. Waislamu wakiongozwa na Saad Waqqas walisonga mbele karibu na Qadisiyya. Saad aliwaweka baadhi ya askari wake mbele ya kikosi kama askari wa safu ya mbele na akamfanya Zuhra bin Abdulla kuwa ni kiongozi (amiri) wa safu hiyo.

Baada ya kupitisha usiku mmoja katika Qadisiyya, Rustam akaenda juu ya kilima kimoja karibu na mahali ambapo jeshi Ia Waislamu lilipiga kambi ili achungue kwa karibu hali ya maadui zake. Ni wazi kwamba Rustam hakushtushwa na idadi, silaha au zana za kivita za Waislamu, lakini hata hivyo moyo wake ukawa unasema kwamba kupigana na watu hao (Waislamu) hakutaleta matokeo mazuri. Usiku huohuo, Rustam akamtuma mjumbe wake kwa Zuhra bin Abdullah kumtaka aje kwake na kupendekeza kwake kufanya suluhu na Waislamu kwa kuwapa pesa kislia kwenda zao.

Zuhra alipofika kwake, Rustam akasema kwa ghururi na kwa kujiona: "Nyinyi mlikuwa jirani zetu, nasi tulikuwa tukiwatendea mema. Nyinyi mlikuwa mkifaidika na neema zetu na wakati mwingine mlipokuwa mkikabiliwa na hatari sisi tulikuwa tukikuhamini na kukulindeni, na historia inashuhudia jambo hili."

Baada ya Rustam kusema maneno hayo, Zuhra akamjibu "Yote hayo uliyoyasema kuhusu zamani ni sahihi, lakini ni lazima wewe utambue jambo hili kwamba leo si jana. Leo sisi si tena watu wenye tamaa ya kidunia. Sasa lengo letu ni Akhera. Ni kweli kama ulivyosema kwamba zamani tulikuwa katika hali hiyo, lakini wakati Mwenyezi Mungu alipomtuma Mtume Wake kwetu hali hiyo ikabadilika.

Mtume ametutaka tumwabudu Mungu Mmoja tu. Tameikubali dini yake. Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume Wake kwamba ikiwa wafuasi wake watayashikilia imara mafundisho yake basi watayashinda mataifa yote. Kila mtu atakayefuata dini hiyo atakuwa mtukufu na kila mtu atakayeipinga atakuwa dhalili na duni."

Rustam akasema: "Tafadali nifafanulie mafundisho ya dini yenu."

"Nguzo na msingi wa dini ni vitu viwili: Kushuhudia kwamba hakuna mungu ila Mmoja tu, na kushuhudia kwamba Muhammad (SAW) ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na yote anayoyasema yanatokana na Mwenyezi Mungu."

"Mafundisho hayo hayana matatizo. Je, kuna mengine?"

"Kuwaacha huru waja wa Mungu kutoka katika utumwa wa wanadamu."

"Hilo pia ni jambo zuri. Je, kuna fundisho jingine?"

"Watu wote wanatokana na baba na mama mmoja tu. Wote ni wana wa Adam na Hawa. Kwa hivyo, wote ni ndugu."

"Hili pia ni zuri sana. Ikiwa tutayaamini na kuyakubali mafundisho hayo yote, mtakwenda zenu?"

"Ndiyo, Wallahi! Hatutokanyaga tena ardhi yenu isipokuwa kwa kuja kufanya biashara au kwa kazi ya dharura, n.k. Sisi hatukukusudia lolote isipokuwa hayo tuliyoyasema."

"Unasema kweli, lakini kuna tatizo moja. Tangu zama za Mfalme Ardeshir ilikuwa ni desturi na kawaida kwetu sisi Wairani kutoikubali dini yenu. Kwa sababu tangu zama hizo ilikuwa ni desturi yetu kuwanyima haki ya kubadilisha kazi wakulima na wafanyakazi ambao wanatoka katika matabaka duni. Ikiwa watu wa matabaka hayo au wana wao watapewa haki ya kubadilisha kazi zao na matabaka yao na wakawa sawasawa na watu watukufu, basi ndimi zao zitakuwa ndefu na wataanza kupigana na watu wa matabaka matukufu. Kwa hivyo, ni afadhali mtoto wa mkulima ajue kwamba ni lazima awe mkulima, na mtoto wa mhunzi ajue kwamba hana haki ya kubadilisha kazi nyingine isipokuwa hiyohiyo ya uhunzi…”

"Sisi leo ni watu tulio bora kwa ajili ya watu wenyewe. Hatuwezi tuwe sawa nanyi na kujiwekea matabaka kama hayo. Tunaamini kwamba amri za Mwenyezi Mungu zitiiwe na kila mtu bila kubaguliwa. Tunaamini kwamba watu wote wameumbwa kutokana na baba na mama mmoja tu na wote ni ndugu. Sisi tunaamini kwamba tuna wajibu wa kuwatendea mema wenzetu. Ikiwa sisi tutatekeleza wajibu wetu basi hatutopata hasara hata kama wao hawatotekeleza wajibu wao. Kutekeleza wajibu humpa mtu kinga."

Baada ya Zuhra kutamka maneno hayo akaenda zake. Rustam akawakusanya majemadari wa jeshi lake na akawaelezea maneno ya Mwislamu huyo, lakini waliyapuuza maneno hayo. Rustam akatuma ujumbe kwa Saad Waqqas kumtaka amtume kwake mjumbe rasmi kwa ajili ya mazungumzo. Saad akataka kutuma ujumbe mmoja kwa ajili ya kazi hiyo, lakini Rabii bin Amir ambaye alikuwapo barazani, aliona hakuna maslahi yoyote, na akasema;

"Wairani wana tabia ya pekee. Ukituma ujumbe mmoja kwao, watachukulia kuwa wao ni watu muhimu sana kwa kuwa sisi tumewatumia ujumbe. Inatosha kumtuma mjumbe mmoja tu."

Rabii mwenyewe akachaguliwa kuwa ni mjumbe kwa ajili ya kazi hiyo.

Rustam akapashwa habari kwamba mjumbe wa Saad bin Waqqas amewasili. Rustam akashauriana na washauri wake wampokee vipi mjumbe wa Waislamu. Wote kwa pamoja wakakubaliana kwamba wampuuze ili kuonyesha kuwa hawamjali hata kidogo mjumbe wa Waislamu.

Rustam akataka kuwatia uchungu Waislamu kwa kuonyesha utukufu na ubora wa Wairani. Akaamrisha kitandikwe kitanda cha dhahabu pamoja na mito iliyoshonwa kwa nyuzi za dhahabu na mazulia aali.

Mjumbe wa Waislamu akaingia hemani akiwa amepanda farasi, akishikilia upanga wake uliofutikwa kwenye ala kuukuu na mkuki uliofungwa kwa kamba ya ngozi. Alipoangalia akafahamu kwamba mapambo hayo yamepambwa ili kumtia yeye uchungu, kwa hivyo, ili kuwaonyesha kwamba Waislamu hawatishiki wala hawajali mapambo hayo, bali wao wana lengo lingine papohapo akaenda mpaka penye baraza Ia Rustam pamoja na farasi wake. Walinzi wakamwambia: "Shuka!" Lakini Rabii hakukubali na akaenda na farasi wake mpaka karibu na kiti cha Rustam, ndipo aliposhuka. Akauchomeka mkuki wake kwenye mto mmoja wa dhahabu na akafunga nao hatamu ya farasi wake. Akajitanda begani gunia kuukuu iliyokuwa kitandiko cha ngamia kuwa kama ni mtandio wake.

Walinzi wakamwambia: "Tukabidhi silaha yako, kisha nenda kwa Rustam." Akjibu: "Sitoi! Nyinyi mlitaka tuwatumieni mjumbe, na mimi ni mjumbe. Ikiwa hamtaki, nitarejea." Rustam akasema: "Mwache aje kama anavyopenda."

Rabii bin Amir akamsogelea Rustam katika kiti chake kwa mwendo wa maringo huku akipiga hatua ndogo ndogo. Akaufanya mkuki wake kama fimbo akichomeka kusudi kwenye mazulia na kuyachana. Alipotaka kukaa akaondoa zulia na akakaa juu ya ardhi. Wakamwuliza "Kwa nini hukai juu ya zulia?" Akajibu: "Mimi sipendi kukaa juu ya mapambo haya."

Mkalimani mahsusi wa Rustam akamwuliza: "Kwa nini umekuja wewe?" Rabii akajibu:

"Mwenyezi Mungu ametutuma ili kuja kuwatoa waja Wake katika shida na dhiki ya dunia na kuwakomboa kutoka katika ukandamizaji na madhila ya madhalimu na kuwaingiza kwenye uadilifu wa Kiislamu. Kwa msingi huu, sisi tunatangaza dini ya Mwenyezi Mungu kwa mataifa yote. Ikiwa watu watakubali kuishi katika himaya dini hii kwa furaha na ufanisi, sisi hatutowaingilia. Lakini ikiwa watakataa, basi sisi tutapigana nao, ambapo ama tutauawa na tutaingia Peponi au tutawashinda maadui."

"Vizuri sana. Tumefahamu maneno yako. Je, inawezekana sasa uakhirishe uamuzi wako ili sisi tuweze kufikiri na tuangalie tuchukue hatua gani?"

"Hapana neno. Unataka fursa ya siku ngapi? Moja au mbili?"

"Siku moja au mbili hazitoshi. Ni lazima sisi tuwaandikie barua viongozi wote wanaohusika; nao hawana budi watachukua muda mrefu kushauriana hadi uamuzi ufikiwe."

Rabii aling'amua kwamba dhamiri yao ilikuwa ni kupoteza wakati, hivyo akawaambia:

"Sunna ya Mtume wetu na mwendo wa viongozi wetu unatufunza kwamba katika hali kama hii si ruhusa kuahirisha zaidi ya siku tatu. Mimi nakupeni fursa ya siku tatu ili mchague mojawapo katika matatu haya: Au muikubali dini ya Kiislamu, nasi tutarejea tulipotoka, na ardhi yenu pamoja na utajiri wake wote itakuwa mali yenu, kwani sisi hatuna tamaa ya mali, utajiri au ardhi yenu. Au mkubali kutoa jizya (kodi maalum). Au muwe tayari kupigana nasi."

"Ni dhahiri kuwa wewe mwenyewe ndiye amiri jeshi hata ukatupa masharti."

"Hapana! Mimi ni mojawapo kati ya watu wa kawaida. Lakini mfano wa Waislamu ni kama viungo vya kiwiliwili kimoja. Wote ni wamoja. Ikiwa mdogo wao kabisa atampa amani mtu mwingine, ni kama kwamba Waislamu wote wametoa amani pia. Wote wanaheshimu mkataba wa amani.”

Rustam aliathirika sana na mkutano huo na akashauriana na majemadari wa jeshi lake kuhusu Waislamu. Akawaambia:

"Mmewaone? Je, katika umri wenu wote mmewahi kusikia maneno ya kishupavu na ya kinaganaga kama ya mtu huyo? Sasa maoni yenu ni nini?"

"Haiwezekani kuikubali dini ya mbwa huyo. Kwani hamkuona nguo kuukuu na zilizochanika alizozivaa?!"

"Wewe nguo unazitakia nini? Angalia fikra na maneno yake, na vitendo na mwendo wake."

Maneno ya Rustam hayakusikilizwa na majemadari hao kwani walijawa na kiburi na majivuno hata hawakuweza kufahamu ukweli ulio dhahiri. Rustam akaona hakuna mtu mwenye fikra na mawazo kama yake. Akafanya tena mazungumzo mengine na wajumbe wa Waislamu, na baada ya kushauriana na majemadari wake wa kijeshi hakuweza kupata ufumbuzi. Vita vikaanza na majeshi yake yakawa ni miongoni mwa majeshi yaliyoshindwa vibaya sana katika historia. Na kutokana na ukaidi wa wenzake, Rustam akapoteza maisha yake katika vita hivyo.