read

Makala hii inaeleza kwa mapana maana ya neno Shi'ah na namna lilivyotumika katika Qur’an na katika Hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

***********
Kwa nini Shi’ah?

“Na shikamaneni kwa Kamba ya Allah nyote, wala msifarikiane…”(Qur’an 3:103)
 
 Neno “Shi’ah” ni kivumishi kinachotumiwa na Waislamu ambao hufuata Maimamu kutoka nyumba ya Mtume (Ahlul Bayt). Neno hilo wanalitumia sio kwa sababu ya utengano au kusababisha migawanyiko miongoni mwa Waislamu. Bali wanalitumia kwa sababu Qur’an hulitumia, Mtume Muhammad (saww) alilitumia, na Waislamu wa mwanzo wamelitumia, hata kabla ya maneno kama Sunni au Salafi hayajakuwepo.

Shi’ah Katika Qur’an

 
Neno “Shi’ah” maana yake “wafuasi; wajumbe wa chama”. Allah ametaja katika Qur’an kwamba, baadhi ya watumishi Wake wema walikuwa Shi’ah wa watumishi Wake wengine wema.

“Na kwa hakika Ibrahim alikuwa miongoni mwa Shi’ah wake” (Qur’an 37:83)
 
“Na akaingia mjini ghafla kwa wenyeji wake, na akakuta humo watu wawili wanapigana, mmoja ni katika Shi’ah wake na mwingine katika maadui zake. Yule ambaye alikuwa Shi’ah wake alimtaka msaada dhidi ya yule ambaye ni adui wake…..(Qur’an 28:15)
 
Hivyo Shi’ah ni neno rasmi lililotumiwa na Allah katika Qur’an Yake kwa ajili ya Mitume Wake wenye vyeo vikubwa halikadhalika na wafuasi wao.
 
Kama mtu ni Shi’ah (mfuasi) wa mtumishi mwema kabisa, basi hakuna kosa lolote kuwa Shi’ah. Kwa upande mwingine, kama mtu akiwa Shi’ah wa dhalimu au muovu, basi atapata hayo yaliyompata kiongozi wake. Qur’an huonyesha kwamba katika Siku ya Malipo watu watakuja katika makundi, na kila kundi litakuwa na kiongozi (Imamu) wake mbele ya Allah. Allah anasema:
“(Kumbuka) siku ambayo tutapo waita kila kikundi cha watu na Imamu wao…” (Qur’an 17:71)
 
 Siku ya Malipo, takdiri (kudra) ya “wafuasi” wa kila kundi hutegemea juu ya takdiri ya Imamu wao (ilimradi kwamba kwa uhakika wamemfuata Imamu huyo). Allah ametaja katika Qur’an kwamba kuna aina mbili za Maimamu:
“Na tuliwafanya Maimamu ambao huita kwenye moto, na Siku ya Qiyamah hawatanusuriwa. Na tukawafuatishia laana katika dunia hii, na Siku ya Qiyamah watakuwa ni watu wanao chusha.” (Qur’an 28:41-42)
 
Qur’an vile vile hukumbusha kwamba kuna Maimamu ambao wameteuliwa na Allah kama Viongozi kwa wanadamu:
 
“Na tukawafanya miongoni mwao Maimamu wanao ongoza kwa amri Yetu wakati walipokuwa na subira, na walikuwa na yakini na Ishara Zetu.” (Qur’an 32:24)
 
Kwa hakika, wafuasi wa kweli (Shi’ah) wa Maimamu hawa watakuwa watakaofuzu katika Siku ya Ufufuo.
 

Shi’ah Na Hadithi

 
Katika historia ya Uislamu neno “Shi’ah” limekuwa likitumika maalumu kwa wafuasi wa Imamu ‘Ali (as). Neno hili halikubuniwa baadae! Mtu wa kwanza kulitumia neno hili alikuwa ni Mjumbe wa Allah mwenyewe, wakati aya ya Qur’an ifuatayo iliposhushwa:
 
“(Na kwa) wale ambao wameamini na kutenda mema, hakika hao ndio bora wa viumbe” (Qur’an 98:7)
 
Mtume akamuambia Ali : “Ni kwa ajili yako wewe na Shi’ah wako.”

Aliendelea kusema: “Naapa kwa yule ambaye anamiliki uhai wangu kwamba mtu huyu (Ali) na Shi’ah wake watapata wokovu Siku ya Ufufuo.”
 
Rejea:
• Jalal al-Din al-Suyuti, Tafsir al-Durr al-Manthur, (Cairo) juzuu 6, uk. 379

• Ibn Jarir al-Tabari, Tafsir Jami’ al-Bayan, (Cairo) juzuu 33, uk. 146

• Ibn Asakir, Ta’rikh Dimashq, juzuu 42, uk. 333, uk.371

• Ibn Hajar al-Haythami, al-Sawa’iq al-Muhriqah, (Cairo) Sura 11, sehemu 1, uk. 246-247.

 
Mtume (saww) alisema: “Ewe Ali! (katika Siku ya Hukumu) wewe na Shi’ah wako mtakuja mbele ya Allah mkiwa mmeridhiwa na mkiwa mmeridhia, na watakuja Kwake maadui zako wakichukiza na shingo zilizo kakamaa (yaani vichwa vyao vimefungwa).”

Rejea:
• Ibn al-´Athir, al-Nihaya fi gharib al-Hadith, (Beirut, 1399), juzuu 4, uk. 106

• al-Tabarani, Mu’jam al-Kabir, juzuu 1, uk. 319

• al-Haythami, Majma’ al-Zawa’d, juzuu 9, namba 14168.

 
Mtume (saww) aliendelea kusema: “Habari njema Ewe Ali! Hakika wewe na Shi’ah wako mtakuwa Peponi.”

Rejea:
• Ahmad Ibn Hanbal, Fadha’il al-Sahaba, (Beirut) juzuu 2, uk. 655

• Abu Nuaym al-Isbahani, Hilyatul Awliya, juzuu 4, uk. 329

• al-Khatib al-Baghdadi, Ta’rikh Baghdad, (Beirut) juzuu 12, uk. 289

• al-Tabarani, Mu'jam al-Kabir, juzuu 1, uk. 319

• al-Haythami, Mu’jam al-Zawa’id, juzuu 10, uk. 21-22

• Ibn ‘Asakir, Ta’rikh Dimashq, juzuu 42, uk.331-332

• Ibn Hajar al-Haythami, al-Sawa’iq al-Muhriqah, (Cairo) Sura 11, sehemu 1, uk. 247.

Lakini Vipi Mtume (Saww) Alitumia Neno Hili Lenye Utenganisho?

 
Je, Mtume Ibrahim alikuwa mtu wa kundi au madhehebu? Vipi kuhusu Mtume Nuh na Mtume Musa? Kama Shi’ah lilikuwa neon la utenganisho au la kikundi Allah asingelitumia kwa Mitume Wake wenye vyeo vikubwa wala Mtume Muhammad (saww) asingewasifia.

Lazima isisitizwe kwamba Mtume (saww) kamwe hakutaka kuwagawa Waislamu katika makundi. Aliwaamrisha watu wote kumfuata Imamu Ali (as) kama wakala wake wakati wa uhai wake, na mrithi wake na Khalifa baada yake. Kwa bahati mbaya wale ambao wamejali matakwa ya Mtume (saww) walikuwa wachache na walijulikana kama “Shi’ah wa Ali”. Mara kwa mara wamepatwa na kila aina ya uonevu na mateso, na waliteseka kuanzia siku ambayo Rehema kwa walimwengu, Mtume Muhammad (saww) alipofariki. Kama Waislamu wote wangetii kile ambacho Mtume (saww) alitaka, basi kusingelikuwepo na kundi lolote au madhehebu ndani ya Uislamu.
Katika hadithi Mtume (saww) alisema:
“Punde tu baada yangu mimi, kutatokea kutokuelewana na chuki miongoni mwenu,wakati hiyo ikitokea, nendeni mkamtafute Ali kwa sababu yeye anaweza kutenganisha haki na batili.”

Rejea:
• Ali Muttaqi al-Hindi, Kanz al-‘Ummal, (Multan) Juzuu 2, uk. 612-Namba 32964.

 
Kuhusiana na aya ya Qur’an iliyonukuliwa hapo mwanzoni, baadhi ya wanachuoni wa ki-Sunni wamesimulia kutoka kwa Imamu Ja’far al-Sadiq (as), Imamu wa sita wa kutoka familia ya Mtume (Ahlul Bayt), kwamba: “Sisi ni Kamba ya Allah ambayo kwayo Allah amesema:” ‘Na shikamaneni kwa Kamba ya Allah nyote pamoja , wala msifarikiane…’”

Rejea:
• al-Tha’labi, Tafsir al-Kabir, chini ya ufafanuzi wa aya 3:103

• Ibn Hajar al-Haythami, al-Sawa’iq, al-Muhriqah, (Cairo) Sura ya 11, sehemu ya 1. uk. 233.

 
Hivyo, kama Allah anakanusha hali ya watu kuwa katika makundi, basi anawashutumu wale ambao wamejitenga kutoka kwenye Kamba Yake, na sio wale walioshikamana nayo!
 

Hitimisho

 
Tumeonesha kwamba neno “Shi’ah” limetumika katika Qur’an kwa ajili ya wafuasi wa Mitume wakubwa wa Allah, na katika hadithi za Mtume (saww) kwa ajili ya wafuasi wa Ali (as). Mtu ambaye hufuata Kiongozi huyu aliyeteuliwa kwa amri ya Mungu, yuko salama kutokana na migogoro katika dini na ameshika Kamba Imara ya Allah, na amepewa habari njema za Peponi.
 
Kutafuta zaidi kuhusu Uislamu sahihi, tembelea:
http//:al-islam.org/faq/
 
 
Translated by: Dr M S Kanju - Tanzania
                        AlItrah Foundation
                        P O Box 1017,
                        Dar es Salaam.
                        Tanzania.
                        Tel 255 22 2110640
                        Email alitrah@daiichicorp.com
                        Website www.alitrah.org