(11). Mabishano Pamoja Na Abu Hanifa

Abu Hanifa alikuwa akiwafundisha wafuasi wake na Bahlul alikuwa ameketi katika kona moja akisikiliza masomo hayo, baina ya mafunzo, Abu Hanifa alisema kuwa yeye hakukubaliana na mambo matatu yaliyoelezwa na Imam Jaafer Sadiq (a.s.), nayo ni:

Kwanza: Imam Jaafer Sadiq a.s. amesema kuwa sheitani ataadhibiwa katika Jahannam (motoni). Kwa kuwa sheitani ameumbwa kwa moto sasa moto utamuumizaje moto huo?

Pili: Yeye amesema kwa sisi hatutaweza kumwona Allah s.w.t. ambapo twajua kuwa kile kilichopo ni lazima kionekane. Hivyo Allah anaweza kuonwa kwa macho.

Tatu: Yeye amesema kila mtenda tendo ndiyo mhusika mwenyewe atawajibika kujibu kwani ametenda mwenyewe. Ambapo sisi (wakina Abu Hanifa) twaamini kuwa kila kitendo kitatokana na Allah na wala mtu hawajibiki.

Abu Hanifa alipoyamaliza kuyasema hayo, Bahlul alichukua rundo moja la udongo na kumlenga Abu Hanifa. Alipoutupa, ulimpiga Abu Hanifa juu ya uso wake, ulileta maumivu makubwa mno. Na hapo ndipo Bahlul alipotimua mbio, lakini wanafunzi wa Abu Hanifa waliweza kumshika Bahlul. Kwa kuwa Bahlul alikuwa akipatana mno na Khalifa, alipelekwa mbele yake, ambapo Khalifa alielezwa hali yote.

Bahlul alisema:
"Aletwe Abu Hanifa ili niweze kumjibu!"

Alipoitwa Abu Hanifa, Bahlul alimuuliza,
"Je, dhambi gani nililokufanyia?

Abu Hanifa alisema:
"Kichwa changu chaumwa sana kwa sababu ya wewe kunipiga rundo la udongo."

Bahlul alimjibu:
"Je waweza kunionyesha maumivu hayo?"

Hapo Abu Hanifa alimwambia:
"Je na maumivu pia yanaweza kuonyeswa?"

Basi Bahlul alianza kumjibu kwa busara: "Wewe mwenyewe umedai kwa kila kitu kilichopo lazima kionekane na umekuwa ukimpinga tena Imam Jaafer Sadiq (a.s.) na vile vile unadai kuwa itawezekanaje kwa Allah kuwapo na asiweze kuonekana?

"Pili madai yako hayafai, kwani inatahidi kuwa kitu cha jinsi moja hakiwezi kukiumiza kitu cha jinsi hiyo (sheitani hana dhambi wala kuchomwa moto) kwani wewe umeumbwa kwa udongo na udongo niliokupiga ni vitu vya jinsi moja."

Tatu, kila tendo linalotokana na Allah, hivyo kwanini wewe unilaumu na kunishtaki mbele ya Khalifa na kudai kisasi kwani umwalumu Allah aliyenisababisha mimi kukupiga ?"

Kwa hayo, Abu Hanifa aliaibika na hakuwa na chaguo lolote isipokuwa kuondoka hapo.