read

Mlango Wa 2: Taratibu Za Kujamiiana Katika Uislam

Kujamiiana na mahusiano ya kijinsia, pamoja na mwenza halali yanatawaliwa na maumbile asilia, na wakati huo huo ni sunnah ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt wake (a.s.). Yametajwa pia kwamba ndio jambo la kuburudisha zaidi maishani. Kikundi cha marafiki na Shi’a wa Imam as-Sadiq (a.s.) wanasimulia kwamba, Imam alituuliza sisi: “Ni nini kinachoburudisha zaidi?” Sisi tukasema: “Kuna vitu vingi vinavyoburudisha.” Imam akasema: “Kile kinachoburudisha zaidi hasa ni kufanya mapenzi na wake zenu.”1

Imesimuliwa vilevile kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Ama katika dunia hii au katika akhera, mtu hajawahi, na wala hatawahi, kupata starehe yenye burudani zaidi kuliko mahusiano ya kijinsia na wanawake, na hakika haya ndio maelezo ya maneno ya Allah (s.w.t.). ndani ya Qur’an, katika Surat Aali Imran, aya ya 14 Yeye ambapo anasema: “Watu wamepambiwa kupenda matamanio pamoja na wanawake na watoto…..”

Halafu yeye akasema: “Hakika, watu wa Peponi hawapendelei sana katika starehe za Pepo zaidi kuliko Nikah;2 si chakula wala vinywaji ambavyo vina buru- dani kama hiyo kwao.”3

Na kuhusu hali nyingine zote za maisha yetu, Uislam unatoa kutupatia sisi taarifa zote muhimu kwa ajili ya maisha ya kijinsia ya mwanaume na mwanamke. Sababu ya hili ni rahisi; Uislam unatambua hulka ya kimaumbile ya mwanadamu, na umeamuru mahusiano ya kijinsia kwa ajili ya starehe na sio kwa ajili ya kuzaa tu. Matamanio ya ngono hayawezi, na hayapaswi kuzuiwa, bali hasa kurekebishwa kwa ajili ya hali njema ya mtu katika ulimwengu huu na akhera. Endapo kanuni na sheria hizi zitazingatiwa kwa makini na kutekelezwa kwa lengo la burudani na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujitenga mbali na maovu ya Shetani, kunahesabiwa kuwa miongoni mwa wema mkubwa kabisa.

Umuhimu Wa Mahusiano Ya Kijinsia

Kuna hadithi nyingi sana zinazobeba ule umuhimu wa uhusiano wa kijin- sia. Una kituo cha ibada na sadaka, na umeitwa kuwa ni Sunnah ya Mtume (s.a.w.w.).

Imam as-Sadiq (a.s.) anasimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alizungumza na mmoja wa masahaba zake katika siku moja ya Ijumaa na akamuuliza: “Je, umefunga leo?” Yule sahaba akajibu. “Hapana.” Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza tena: “Je, umetoa chochote leo kama sadaka?” Akajibu, “Hapana.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Basi nenda kwa mke wako na hiyo ndio sadaka hasa kwake yeye.”4
Katika hadithi nyingine, Imam as-Sadiq (a.s.) anasimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwambia mtu mmoja: “Wewe umefunga leo?” Akajibu akasema, “Hapana.”

Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza: “Je, umekwenda kutembelea mgonjwa yoyote?” Akajibu, “Hapana.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza: “Je, umekwenda kusindikiza jeneza?” Akajibu, “Hapana.” Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza: “Je, umetoa chakula kwa mtu masikini?” Akatoa majibu ya kinyume tena. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Nenda kwa mke wako, na kumwendea mke wako ni sadaka (Mwendee ili upate malipo kwa ajili ya matendo yote hayo).”5

Muhammad bin Khalad anasimulia kutoka kwa Imam ar-Ridhaa (a.s.): “Mambo matatu ni kutoka kwenye sunnah za manabii watukufu na mitume wa Allah (s.w.t.)., na haya ni kutumia manukato, kukata nywele na kijiingiza sana kwenye mahusiano ya ndoa na wake zao.”6

Kukaa mbali na mahusiano ya kindoa ya mtu na mke wake ni matokeo ya minong’ono ya Shetani, na kuna matokeo ya kinyume mengi sana kama vile mabishano na chuki baina ya mume na mke wake.

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): Mabibi watatu walikwen- da kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kulalamika. Mmoja wao akasema: “Mume wangu huwa hali nyama.” Yule mwingine akasema: “Mume wangu hanusi manukato na wala hatumii manukato.” Na yule wa tatu akasema: “Mume wangu mimi hasogei karibu na wanawake (yaani, hajishughulishi na kujamiiana).”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), akiwa hana furaha, katika namna ambayo kwamba joho lake lililobarikiwa lilivyokuwa likiburuzika ardhini, aliondoka na kwenda msikitini na akiwa juu ya mimbari, alimtukuza Mwenyezi Mungu na kisha akasema: “Ni nini kimetokea, kwamba kikundi cha wafuasi wangu hawali nyama, au hawatumii manukato, au hawawaendei wake zao? Ambapo mimi ninakula nyama, ninatumia manukato, na pia ninamwendea mke wangu. Hii ndio sunnah yangu, na mtu yoyote anayekwenda kinyume na sunnah hii huyo hatokani na mimi.”7

Imam as-Sadiq (a.s.) vilevile amesimulia: Mke wa Uthman bin Ma’dhun alikwenda kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kila siku Uthman anafunga na wakati wa usiku anajishughulisha katika Swala.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akaokota makubazi yake na kwa hasira akaenda kwa Uthman (kiasi kwamba hakun- goja kuvaa makubazi yake) na akamkuta katika hali ya Swala.

Kwa vile Uthman alimuona Mtume (s.a.w.w.) aliiacha Swala yake. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamhutubia akasema: “Allah hakunituma mimi kuwa sufii (anayejitenga peke yake), ninaapa Wallahi, kwamba hilo limenichochea mimi kwenye dini hii safi, yenye imani halisi na rahisi, mimi ninafunga, ninaswali na ninakwenda kwa mke wangu, na yeyote anayependa desturi yangu, ni lazima ashikamane na sunnah yangu na mwenendo wangu, na Nikah8 ni sunnah yangu.9

Umuhimu Wa Kumridhisha Mke Wako

Kumridhisha mke wake mtu ni jambo muhimu sana katika Uislam, kama lilivyoonyeshwa na hadithi ifuatayo hapo chini; kwa kweli, kukosa kuridhika kwa kipindi cha muda mrefu kunaweza kusababisha kukosa ashiki na chuki ya mke kwa mumewe.

Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): Wakati yeyote kati yenu anapotaka kulala na mke wake, basi asimharakishe kwani wanawake wanayo mahitaji pia.10 Ni muhimu kwa mume kutambua kwamba hamu ya kujamiiana ya mwanamke inachukua muda mrefu kujionyesha yenyewe, lakini mara inapokuwa imevutika, inakuwa na nguvu sana, ambapo kwa mwanaume ni rahisi, anapata ashiki haraka sana na vilevile anaweza kuridhishwa haraka sana.
Mwisho, inatia moyo kuona kwamba umuhimu uliowekwa na Uislam juu ya kuridhika kwa wote, mwanaume na mwanamke ni kiashirio cha wazi cha uadilifu na wema wa Mwenyezi Muntu (s.w.t.), kwa kweli, imerudia kukaririwa ndani ya Qur’ani kwamba mwanaume na mwanamke waliumbwa kutokana na nafsi moja,11 na huu ni mfano mmoja tu wa hili.

Vitendo Vilivyopendekezwa

Hakuna kanuni maalum kwa ajili ya kujamiiana; chochote ambacho kinawaridhisha wawili hao ni sawa, kadhalika, chochote ambacho hakiwaridhishi wawili hao ni lazima kiepukwe; kikwazo pekee kwenye kanuni hii ni kile ambacho Shari’ah inakikataza kwa uwazi kabisa. Hata hivyo, kuna vitendo kadhaa vilivyopendekezwa ambavyo, kama vikifuatwa, vitatarajiwa kuongozea kwenye hali ya kuridhisha zaidi.

Kabla Ya Kujamiiana

1. Piga mswaki meno yako na tafuna kitu chenye harufu nzuri ili kuondoa harufu mbaya yoyote mdomoni. Kadhalika, jaribu kutokula vyakula vyenye harufu isiyopendeza kabla ya kukutana pia, kama vile kitunguu na kitunguu saumu.

2. Hakikisha unanukia vizuri – harufu safi zaidi ni ile ya mara tu baada ya kuoga au kujisafisha kwa haraka, na harufu mbaya zaidi ni ile ya jasho! Hususan wanawake wanahisia kali sana juu ya harufu.

Matumizi ya manukato, mafuta mazuri na vitu kama hivyo vinapendekezwa sana, ingawa ni muhimu sana kutambua kwamba kutumia vitu vya asili ni bora sana, ambavyo havina mchanganyiko na kemikali ambazo zinaweza kusababisha madhara mwilini.

Hasa, wanja (kuhl) umependekezwa sana juu ya wanawake. Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.): “Kupaka wanja kuyazunguka macho kunakipa kinywa harufu nzuri, na kunazifanya kope za macho kuwa na nguvu na kunaongeza nguvu na mvuto wa kujamiiana.12

Imesimuliwa pia kutoka kwa Imam as-Sadiq (s.a.): Kupaka wanja nyakati za jioni kuna manufaa kwenye macho na nyakati za mchana ni katika sunnah.13

Jalizo: Ingawa hadithi zinapendekeza matumizi ya wanja (kuhl), haziruhusu matumizi
yake katika maeneo ambayo yanaweza kuonekana kwa wanaume na yakaweza kuwa chanzo
cha mvuto na ushawishi.

Unyegereshano (Kutiana Ashiki)

Umuhimu Wa Unyegereshano

Kama ilivyosisitiziwa mapema, mume kumridhisha mke wake ni muhimu sana, na kujiingiza kwenye kujamiiana haraka na kwa pupa sio njia sahihi. Kuna wastani wa tofauti ya dakika nane kati ya muda ambao mume na mke wanafikia kileleni; mwanaume kwa kawaida anachukua dakika mbili kufikia kileleni na mwanamke anachukua dakika kumi kufikia kileleni. Kwa hiyo, ili kumridhisha kikamilifu mke wake, mwanaume lazima ampapase na kumchezea kimapenzi na kujishughulisha katika kunyegereshana (kutiana ashki) ili wote wafikie kileleni kwa pamoja kwa wakati mmoja.Uislam unatilia mkazo sana umuhimu wa unyegereshano, kama unavyoashiriwa katika hadithi zifuatazo hapa chini:

Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Usijishughulishe katika kujamiiana na mkeo kama kuku; bali kwanza kabisa jishughulisha katika kutiana ashiki kwa unyegereshano pamoja na mke wako na kuchezeana naye halafu ufanye mapenzi naye.”14

Imesimuliwa pia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Starehe na michezo yote haina maana isipokuwa kwa mitatu tu: Upanda farasi, kurusha mishale na unyegereshano na mke wako, na hii mitatu ni sahihi.”15

Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): “Yeyote anayetaka kuwa karibu na mke wake lazima asiwe na papara, kwa sababu wanawake kabla ya kuji- ingiza kwenye tendo la kufanya mapenzi lazima wajiingize kwenye unyegereshano ili kwamba wawe tayari kwa ajili ya kufanyiwa mapenzi.16

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Malaika wa Mwenyezi Mungu na wale ambao ni mashahidi juu ya matendo yote ya wanadamu wanawaangalia katika kila hali isipokuwa wakati wa mashindano ya kupanda farasi na ule wakati ambapo mwanaume anajiingiza katika kujishughulisha na unyegereshano na mke wake kabla hawajajihusisha katika kujamiiana.” 17

Taratibu Za Kunyegereshana

Kuna vikwazo vichache sana kwenye taratibu zinazotumika katika unyegereshano; kupigana mabusu, kukumbatiana na kadhalika yote haya yanaruhusiwa. Hapa chini ni baadhi ya mbinu zinazofaa kwenye taratibu maalum:

A) Upapasaji Kwenye Matiti

Imesimuliwa kutoka kwa Imam ar-Ridhaa (a.s): “Usijiingize kwenye kujamiiana isipokuwa kwanza ujishughulishe katika unyegereshano, na ucheze naye mkeo sana na kumpapasa matiti yake, na kama ukifanya hivi atazidiwa na ashiki (na kusisimka kwa upeo kamilifu) na maji yake yat jikusanya. Hii ni ili ule utoaji wa majimaji uchomoze kutoka kwenye mati- ti na hisia zinakuwa dhahiri usoni mwake na kwenye macho yake na kwamba anakuhitaji kwa namna ileile kama wewe unavyomhitaji yeye.” 18

B) Mapenzi Ya Mdomo (Maongezi)

Imam al-Kadhim (a.s.) aliulizwa: “Kuna tatizo kama mtu atabusu sehemu za siri za mke wake?” Imam alijibu akasema: “Hakuna tatizo.”19

DOKEZO: Ingawa kupiga punyeto (kujisisimua mwenyewe uchi wako mpaka ukatoa manii) kunakatazwa, katika suala la watu waliooana hakuna tatizo kama mke anasisimua tupu ya mume wake mpaka kutokwa na manii, au mume anasisimua tupu ya mke wake hadi anafikia kilele cha raha ya kujamiiana. Hili linaruhusiwa kwa sababu haliingii kwenye (kujisisimua mwenyewe;) ni kujisisimua kwa njia ya mwenza halali

C) Mengineyo

Iliulizwa kwa Imam as-Sadiq (a.s.) “Endapo mtu atamvua nguo mke wake (na kumuacha uchi) na halafu akawa anamwangalia, je kuna tatizo lolote katika hilo?” Yeye akajibu akasema: “Hapo hakuna tatizo, hivi kuna stare- he bora kuliko hiyo ambayo inaweza kupatikana?” Likaulizwa swali jingine tena: “Kuna tatizo lolote iwapo mume atachezea sehemu za siri za mke wake?”

Imam akajibu: “Hakuna tatizo, kwa sharti kwamba hatumii kitu chochote mbali na viungo vya mwili wake (asitumie kitu cha nje cha ziada).”

Halafu tena Imam akaulizwa: “Kuna tatizo lolote kufanya ngono ndani ya maji?”
Imam akajibu: “Hakuna tatizo.” 20

Dokezo: Hadithi hiyo hapo juu inasisitizia makatazo ya kutumia vitu vya nje.

Baada Ya Kujamiiana

1. Ni mustahabu kwamba josho la janaba ‘Ghusl al-Janaabat’ linafanywa mara tu baada ya tendo la ndoa, na linapochukuliwa mapema zaidi ndio bora. Vilevile, kama mtu angependa kufanya ngono zaidi ya mara moja katika usiku mmoja, ni bora kwamba kila mara waoge josho la janaba. Hata hivyo, kama hilo litakuwa haliwezekani kutendeka, inapendekezwa kwamba mtu atawadhe kabla ya kila tendo.21

2. Mara tu baada ya kumaliza tendo la ngono, mume hana budi kuoga josho na wakati huohuo ale sehemu ya nta ya nyuki (inayosifika kwa kuponya aina zote za majeraha, hususan mipasuko na mivunjiko) iliyochanganywa na asali na maji au iliyochanganywa na asali safi, halisi, kwani hii itafidia yale majimaji yaliyopotea.22

3. Kama nguvu za kiume za mtu zikiisha haraka baada tu ya kujamiiana, hana budi kujipasha mwili moto na kisha kulala.23

4. Mume na mke hawana budi kutumia mataulo tofauti katika kujisafisha wenyewe. Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba kama litatumika taulo moja tu, hii itasababisha uadui na utengano baina ya wawili hao.24

Vitendo Visivyopendekezwa

Vitendo Vinavyoleta Karaha (Makruuh)

1. Liwati!

Kuna baadhi ya Wanavyuoni wanaosema kuwa Liwati inaruhusiwa kwa ridhaa ya mke, lakini ni kauli zisizo na nguvu, na pia ni kitendo kinachochukiwa sana!

Zayd ibn Thabit anasimulia kwamba mtu mmoja alimuuliza Imam Ali (a.s.): “Je, unaweza kumsogelea mkeo nyuma kwake?” Imam Ali (a.s.) akajibu akasema: “Likatae, lichukie hilo liwe kinyaa kwako! Mwenyezi Mungu anakushusha kwa njia hii (ya kumwingilia mwanamke). Hukuyasikia maneno ya Mola Wako kwamba imesimuliwa kutoka kwa Lut ambaye alisema kuwaambia kaumu yake:

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُمْ بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِنَ الْعَالَمِينَ {80}

“Kulikoni! Mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa (ufasiki) huo katika walimwengu? (Al-A’araf; 7:80). 25

Kuna baadhi ya watu wanaolihalalisha tendo hili kwa kutumia aya ya Qur’ani Tukufu ifuatayo:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ ۖ {223}

“Wanawake ni mashamba yenu, basi yaendeeni mashamba yenu kwa namna muitakayo …”
(Al-Baqarah; 2:223).

Hata hivyo, Imam as-Sadiq (a.s.), katika tafsiri yake juu ya aya hiyo ya Qur’ani hapo juu anasimulia kwamba: “Madhumuni ya aya hii ni kwamba kujamiiana hakuna budi kufanyika kutokea mbele, kwani sababu ambayo kwamba mwanamke katika aya hii amefananishwa na shamba linalotoa mavuno (kutokea juu ya udongo) ambao ni kama tu kule mbele kwa mke kwa sababu huku ndiko ambako kwamba mtoto hutokea kupatikana na kuja ulimwenguni humu.”26
Abuu Basiir anasimulia kwamba yeye alimuuliza Imam kwamba ni nini hukmu ya mtu anayemwendea mke wake nyuma. Imam alilichukulia tendo hili kutokubalika na akasema: “Kaa mbali na nyuma kwa mkeo, na maana ya aya hii tukufu ya Surat al-Baqarah hapo juu sio kwamba unaweza kumwingilia mkeo kutokea popote unapotaka, bali haswa ni kwamba huna budi kufanya ngono, na kwa hiyo maana ya aya hiyo ni kumkurubia mkeo kwa wakati wowote uupendao kufanya hivyo.”27

2. Kuwa Na Qur’ani Au Majina Ya Allah (S.W.T.) Mwilini Mwako

Imesimuliwa kutoka kwa Ali, mtoto wa Imam as-Sadiq (a.s.): Nilimuuliza ndugu yangu Imam Kadhiim (a.s.): “Je, mtu anaweza kujamiiana na akaenda bafuni wakati akiwa na pete mkononi mwake yenye jina la Allah au aya ya Qur’ani iliyoandikwa juu yake?” Imam alijibu akasema: “Hapana – hilo ni makuruhu.”28

3. Kufanya Mapenzi (Ngono) Kwa Kusimama Wima

Inasimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Mume na mke wasije wakajamiiana kama punda wawili waliong’ang’aniana pamoja, kwa sababu kama ikiwa namna hiyo, malaika wa rehma watakaa mbali nao na neema ya Mwenyezi Mungu itaondolewa kutoka kwao.29

4. Kujamiiana Wazi (Bila Kujifunika Nguo)

Imesimuliwa kwamba Muhammad ibn al-Ais alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Je, inaruhusiwa kumwendea mke wangu nikiwa uchi kabisa (yaani kujamiiana bila kujifunika)?” Imam alijibu akasema: “Hapana, usifanye jambo kama hilo…..”30

5. Kushughulika Na Ngono Chini Ya Anga

Imesimuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.): “Allah anazichukia tabia 24 kwa ajili yenu, enyi watu, na amekukatazeni kutokana nazo; moja ya tabia hizi ni kujamiiana chini ya anga.”31

6. Kushughulika Na Kujamiiana Panapokuwa Na Watu Wengine (Na Wanaweza Kuwasikia Na/Au Kuwaona) Ndani Ya Nyumba

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.): “Ni makuruhu kwamba mtu ashughulike katika kujamiiana na mke wake kama, pamoja na kuwepo kwao, kuna mtu mwingine pia ndani ya nyumba hiyo.32

Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Twaeni tabia tatu kutoka kwa kunguru; kujamiiana kwa siri, kwenda kutafuta riziki mwan- zoni mwa asubuhi, na akili na hadhari dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza.” 33

7. Kujishughulisha Na Kujamiiana Mbele Ya Mtoto Mdogo

Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): “Mtume amekataza kwamba mtu amwendee mke wake (kwa ajili ya kujamiiana) na mtoto katika susu lake anaweza kuwaona. 34

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.): “Epukana na kujamiiana katika sehemu ambayo panaweza kuwa na mtoto anayeweza kuwaoneni.35

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Jiepushe na kwenda kulala (kwa ajili ya kujamiiana) na mke wako wakati ambapo mtoto anaweza kuwaoneni, kwani Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alijua sana hasa kwamba kitendo hiki ni Makruhu na cha kuaibisha sana.”36

8. Kushughulika Na Kujamiiana Ndani Ya Jahazi, Ufukweni 63Au Barabarani

Imesimuliwa katika hadithi kwamba kujamiiana ndani ya jahazi au barabarani kunaishia kwenye laana ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ya Malaika kuwa juu yako mtu.37

Imesimuliwa katika hadithi nyingine kutoka kwa as-Sakuni kwamb Imam Ali (a.s.) aliwapita wanyama wawili waliokuwa wakijamiiana mahali njia ya watu wengi. Imam aligeuka mbali nao.

Ikaulizwa: “Ewe Amirul-Mu’minin, kwa nini uligeukia pembeni mbali nao?” Imam (a.s.) akajibu akisema: “Sio sahihi kwamba mkaribiane katika njia ya watu kama wanyama hawa; kitendo kama hicho kimekatazwa na kifanyike mahali ambapo si mwanaume au mwanamke awezaye kuona.” 38

9. Kuelekea, Au Mtu Kukipa Mgongo Qiblah

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amekataza watu kujamiiana wakati wakiwa wameelekea Qiblah, au mtu mgongo wake kuelekea Qiblah, na amesema kwamba endapo kitendo kama hicho kikifanyika, kinaleta matokeo ya laana ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Malaika na wanadamu wote kuwa juu yako mwenye kufanya hivyo.39

Dokezo: Ikiwa pale unapokaa wima kutoka kwenye hali ya kulala, uso wako unaelekea Qiblah, hii inafahamika kama kuelekea Qiblah, na kinyume chake (yaani na mgongo pia).

10. Kukataa Kujamiiana (Kwa Sababu Mbalimbali)

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.): Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema kuwaambia wanawake: “Msirefushe Swala zenu kiasi kwamba ikawa ni kisingizio cha kutokwenda kulala (kwa ajili ya kujamiiana) na waume zenu.”40

Nyakati Zinazopendekezwa

Nyakati Za Wajibu

1. Ikiwa Kuna Hofu Ya Haramu (Iliyokatazwa)

Endapo mtu anahofia kwamba anaweza kushindwa na tamaa zake za kingono na minong’ono ya Shetani na akaweza kujiingiza katika vitendo vya haramu, ni wajibu kwamba wajichunge na wajilinde nalo hili.41

Kama mtu yuko peke yake, ni lazima afunge ndoa na hivyo kujiweka mbali na vitendo vyovyote vinavyowezekana kuwa vya haramu (vilivyokatazwa).

Imesimuliwa kutoka kwa Ayatullah Khomeini (r.a.) “Ni faradhi kwa mtu ambaye, kwa sababu ya kutokuwa na mke ataangukia kwenye haram, afunge ndoa.” 42

2. Mara Moja Kwa Kila Miezi Minne

Mtu ni lazima apate kujamiiana na mkewe kijana angalau mara moja katika miezi minne. Hii ni moja ya haki za ndoa za mke na wajibu huo unabaki kufanya kazi isipokuwa ima kama una madhara kwa mume, unahusika na kutumia jitihada za ziada zisizo za kawaida, au mke kusamehe haki yake au masharti ya awali kama hayo yalikuwa yamewekwa na mume wakati wa kufunga ndoa. Haina tofauti kama mume yuko mbali safarini ama yupo nyumbani.

Safwan ibn Yahya alimuuliza Imam ar-Ridhaa (a.s.): “Mtu anaye mke kijana na akawa hajamkaribia kwa kiasi cha miezi, au hata mwaka. Sio kwa sababu anataka kumtaabisha yeye (kwa kukaa mbali naye), bali hasa ni janga fulani limewashukia. Je, hili linahesabiwa kama ni kosa?”

Imam akajibu akasema: “Endapo atamwacha kwa kiasi cha miezi minne, hilo linahesabiwa kama
ni dhambi.”43

Nyakati Zinazopendekezwa (Mustahab)

Kujamiiana, kama kutafanywa katika namna inayoruhusiwa, basi wakati wote kunakuwa ni mustahabu. Hata hivyo, kuna nyakati ambazo kunapendekezwa zaidi.

1. Wakati mke anapokuhitaji kutoka kwa mumewe.
2. Wakati mume anapokuwa amevutiwa na mwanamke mwingine.44

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) “Mtu yoyote atakayeona mwanamke na akavutiwa naye ni lazima aende kwa mke wake na aka- jamiiane naye, kwa sababu kile ambacho yule mwanamke mwingine ana- cho, na mke wako pia anacho, na mtu asimwachie nafasi Shetani katika moyo wake.

Na endapo mtu hana mke, ni lazima aswali Swala ya rakaa mbili, amtukuze sana Allah (s.w.t.). na kumswalia Mtume – kumtakia rehma yeye na kizazi chake na amuombe Mwenyezi Mungu amjaalie kumpa mke muumini na mchamungu, na kwamba Yeye Allah (s.w.t.). amfanye asiwe mwenye kuhitaji yaliyoharamishwa.45

Nyakati Zisizopendekezwa

Nyakati Haram – Zinazokatazwa

1. Wakati wa heidhi (siku za mwezi za mwanamke):

Allah (s.w.t.). anaeleza ndani ya Suratul-Baqarah, aya ya 222 kama ifuatavyo:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ {222}

“Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie: Huo ni uchafu, basi jitengeni na wanawake (wakiwa) katika hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watakapotoharika …..” (Al-Baqarah; 2:222).

Endapo mtu anayejamiiana na mke wake akagundua kwamba kipindi chake cha hedhi kimeanza, basi na ajiondoe na kujitenga naye mara moja.

Ndani wa kipindi cha hedhi, vitendo vingine, mbali na kujamiiana vinaruhusiwa kufanyika kama inavyoonyeshwa na hadithi ifuatayo hapa chini:

Mu’awiyah ibn Umar anasimulia kwamba, yeye alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Ni nini kinachoruhusiwa kwa mwanaume wakati mwanamke anapokuwa kwenye hali ya hedhi?”
Imam akajibu akasema: “Mbali na sehemu zake za siri (yaani, mwili wote uliobakia isipokuwa sehemu zake za siri tu). 46

Imran ibn Qanzali anasimulia kwamba yeye alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Ni vipi mwanaume anavyoweza kufaidika kutoka kwa mwanamke ambaye yuko kwenye hali yake ya hedhi?” Imam akajibu akasema: “Yale mapaja mawili (ya mwanamke huyo).” 47

Hata hivyo, ingawa mwili wote uliobakia, wa mwanamke (ukiachilia mbali sehemu zake za siri) unaruhusiwa kwa mume, lile eneo tokea kitovuni hadi magotini ni makuruhu (haipendekezwi kufikiwa);48 kwa hiyo inashauriwa sana kwamba mume azikwepe sehemu hizi vile vile.

Ni muhimu kutambua kwamba haipendekezwi kujishughulisha na ngono baada ya kwisha kwa hedhi. Hata hivyo, kama ni lazima, mwanamke anapaswa kuoga kwanza.49

Mwenyezi Mungu analieleza hili katika muen- delezo wa aya hiyo hapo juu: “Na wanapokuwa tohara, basi waingilieni kama alivyokuamuruni Mwenyezi Mungu.” (Al-Baqarah; 2:222).

2. Wakati wa Nifaas 50

3. Wakati wa kufunga katika mwezi wa Ramadhani.51

4. Wakati katika hali ya Ihraam na kabla ya kuswali swala ya Tawafun Nisaa.52

5. Pale ambapo inaweza kusababisha madhara makubwa kwa amma mwanaume au mwanamke. Kujamiiana kunaruhusiwa endapo hakuwezi kuleta madhara makubwa.53

Nyakati Makuruhu

1. Katika Hali Ya Ihtilaam

Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Ni Makruh kwamba mwanaume ambaye amekuwa Muhtalim (yaani, aliyekuwa katika hali ya janaba akiwa usingizini – kwenye ndoto) amwendee mkewe (ili kujamiiana naye) akiwa katika hali hii, isipokuwa pale atakapooga kwa ajili ya ihtilaam yake.”54

2. Wakati Wa Safari, Na Kukiwa Na Uwezekano Wa Kukosekana Maji

Imesimuliwa kutoka kwa Is’haaq ibn Ammaar: “Nilimuuliza Imam as- Sadiq (a.s.): “Mwanamume amefuatana na mke wake wakati wa safari, lakini hakupata maji yoyote kwa ajili ya kufanyia Josho. Je, anaweza kulala (kujamiiana) na mke wake?” Imam akajibu: “Hilo silipendi kama akifanya hivyo nalo ni makruh, isipokuwa kama akiwahofia kwamba kama hatakiendea kilicho halali yake, ataangukia kwenye kilichoharamishwa.”55

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Kadhim (a.s.): “Silipendi lile jambo la kwamba mtu anapokuwa safarini, ambaye hana maji halafu anajishughul- isha katika kujamiiana, isipokuwa kama anahofia madhara.” 56

(Katika hali kama hizi, kwa mujibu wa kanuni za Fiqhi, mtu anaweza kutayamman badala ya josho ili kuweza kuswali).

3. Usiku Wa Kupatwa Kwa Mwezi Na Mchana Wa Kupatwa Kwa Jua

Usiku mmoja, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa karibu na mmoja wa wake zake na jioni ili kukatokea kupatwa kwa mwezi, na hakuna lolote lililotokea baina yao. Mke wa Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Kwa nini huna furaha na mimi usiku wote wa leo?” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akajibu: “

Ni nini unachokisema, jioni hii ilikuwa ni usiku wa kupatwa kwa mwezi na mimi ninajua kuwa ni Makruh kwamba nipate starehe usiku huu, kwa sababu Mwenyezi Mungu anakikaripia kikundi cha watu wasiojali na wasio makini kwenye Hujja na ishara Zake, na amewaelezea katika namna ifuatayo:

وَإِنْ يَرَوْا كِسْفًا مِنَ السَّمَاءِ سَاقِطًا يَقُولُوا سَحَابٌ مَرْكُومٌ {44}

“Na kama wakiona kipande cha mbingu kikianguka husema: ni mawingu yanayobebana.”
(At-Tuur: 52:44) 57

4. Baina Ya Subh As-Sadiq (Adhana Ya Alfajir) Na Kuchomoza Kwa Jua Na Kati Ya Kuzama Jua Na Kutoweka Kwa Wekundu Wa Mbingu

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Kupata kuwa na janaba wakati wa wekundu wa jua linapochomoza na wekundu wa jua linapozama ni Makruh.”58

5. Wakati Wa Tetemeko La Ardhi (Na Matukio Mengine Yanayolazimu Kuswali Salat Al-Ayaat)

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.) kwamba: “Mtu ambaye haachi raha na starehe katika wakati wa Ishara za Mwenyezi Mungu zinapodhihiri, anatokana na wale watu ambao wamezichukulia ishara zake Mwenyezi Mungu kuwa ni kama mzaha.”59

Mwili Wenye Afya Njema

Mwili wenye afya njema hurusu kuwa na maisha ya uhusiano timamu wa kijinsia. Vitendo kadhaa vimependekezwa katika Uislam, na kama maelekezo haya yatafanyiwa kazi, yatasababisha kuwa na mwili safi na wenye afya njema.

Mambo Yanayopendekezwa:

Mambo Yanayopendekezwa: 60

1. Kusafiri

2. Kufunga swaumu

3. Kula zabibu kavu 21 kwenye tumbo tupu lenye njaa

4. Kunywa maji ya mvua. 61

5. Kuswali Swala ya usiku Salaat al-Layl.

6. Kuosha mikono kabla na baada ya kula.

7. Kujisaidia pale inapohitajika haja ya choo.

8. Kuosha miguu (nyayo) kwa maji baridi baada ya kuoga.

9. Kuulinda mwili kutokana na baridi ya majira ya kupukutika kwa majani ya miti bali sio kuukinga na baridi ya wakati wa majira ya kuchipua (yaani kuvaa nguo nzito wakati wa kupukutika na nyepesi wakati wa majira ya kuchipua).

10. Kupata kiwango cha kutosha cha mapumziko.

11. Kula binzari nyembamba (aniseed) na tende.

12. Kutafuna vyema chakula chako.

13. Kula chakula pale tu unapojisikia njaa na kuepuka kula wakati umeshiba.

14. Kula chakula kiwango cha kiasi na hivyo kunywa kiasi cha kadiri

Matumizi Ya Mafuta Ya Kuchulia

Matumizi Ya Mafuta Ya Kuchulia62

Hususan mafuta ya kuchulia ni yenye manufaa sana kwa mwili wenye afya njema na vilevile ashiki ya kujamiiana, kiasi kwamba Maimam (a.s.) wamesimulia hadithi juu ya jambo hili:

Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba: “Kuupaka mwili na mafuta ya kuchulia kunalainisha ngozi, kunaboresha hali, kunafanya mtiririko wa maji na vimiminika ndani ya mwili kuwa rahisi, kunaondoa zahama, makunyanzi, afya mbaya na ugumu wa kipato na kunaleta nuru kwenye uso.”63

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.) kwamba: “Kuupaka mwili mafuta ya kuchulia wakati wa jioni ni chanzo cha mzunguko katika mishipa ya damu na (hili) huipa nguvu tena hali ya ngozi na kung’arisha uso.”

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba: “Angalau mara moja kwa mwezi, au mara moja, mbili kwa wiki, pakaza mafuta kwenye mwili wako. Hata hivyo, kama wanawake wakiweza, ni lazima wajaribu kutumia mafuta kwenye miili yao kila siku.

Aina Za Mafuta Zifuatazo Zimependekezwa

1. Mafuta Ya Urujuani

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Mafuta ya urujuani ni mafuta ya nguvu: yasugue katika mwili wako ili yaweze kuondoa mau- mivu ya kichwa na macho.”

Mtu mmoja alianguka chini kutoka kwenye ngamia wake, na wakati maji yalipoanza kutoka kwenye pua yake, Imam as-Sadiq (a.s.) akamwambia: “Mwagia mafuta ya urujuani juu yake.” Yule mtu alipofanya hivyo, alitibika na akapona vizuri kabisa. Baada ya hapo Imam akasimulia: “Mafuta ya urujuani wakati wa kipupwe ni ya vuguvugu na wakati wa kiangazi ni yanakuwa poa kidogo64 kama watu wangeelewa yale maufaa ya mafuta haya, wangekunywa kiasi chake kikubwa; mafuta haya yanaondoa maumivu na kutibia na kuponya pua.”

2. Mafuta Ya Willow (Catkin)

Mtu mmoja alikuja kwa Imam as-Sadiq (a.s.) na kulalamika juu ya mikono na miguu iliyoatuka na kuwa na mikwaruzo. Imam akamwambia: “Chukua pamba, iloweke kwenye mafuta ya mti wa willow na uiweke hapo katikati (ya muatuko/mpasuko).” Yule mtu alipofanya kitendo hicho, yale maumivu yakatoweka.

3. Mafuta Ya Yungiyungi

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Mafuta ya yungiyungi yana tiba kwa magonjwa 70, na ni bora kama itakuwa yungiyungi nyeupe, ambayo inajulikana pia kama Jasmini ya Kiarabu.”

4. Mafuta Ya Zeituni

Kama mafuta ya zeituni yatachanganywa na asali na yakanywewa badala ya maji kwa muda wa siku tatu, yanaongeza nguvu ya kijinsia (za kujamiiana). Kama mafuta ya zeituni yatapakwa kwenye nywele, yanazuia zisikatike au kuota mvi nyeupe. Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Kula mafuta ya zeituni kunaongeza shahawa na nguvu ya uwezo wa kujamiiana.”65

Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Hasa kula mafuta ya zeituni kwa sababu dawa hii inatibia nyongo, inaondoa kikohozi, inaimarisha neva, inaponya maumivu, inafanya akhlaq kuwa nzuri, inafanya kinywa kunukia vizuri na inamuondolea mtu huzuni.”66

Imesimuliwa pia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Kula mafuta ya zeituni na yasugue mwilini, kwani yanatokana na mti uliobarikiwa.”67

Vile vile imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Mtu yoy- ote anayekunywa mafuta ya zeituni na kuyasugua mwilini mwake, Shetani hatamsogelea karibu yake kwa asubuhi arobaini.”

5. Mafuta Mengineyo

Mume na mke ambao wanataka kuongeza kiwango chao cha mshughuliko wa kujamiiana, lakini wakawa hawajui ni nini wanalazimika kukifanya, kadhalika watu ambao wangependa kufikia starehe zaidi ya kujamiiana, wanapaswa kutumia mafuta ya kuchulia kama vile zeituni ya Kiarabu, mafuta ya nazi, mafuta ya urujuani na mafuta ya zeituni.68

Mambo Yasababishayo Madhara Mwilini Kuhusiana Na Kujamiiana

1. Kujamiiana mwanzoni mwa usiku, iwe wakati wa kiangazi ama wa kipupwe, kunasababisha madhara kwenye mwili kwa sababu wakati huo tumbo na mishipa ya damu kwa kawaida inakuwa imejaa. Kujamiiana kunaweza kusababisha chango (msokoto wa tumbo bila kuharisha), kupooza (kwa uso), jongo (gout), mawe na kutiririka kwa mkojo, henia na udhaifu wa macho.69

Kwa hiyo, kushughulika katika kujamiiana mwishoni mwa usiku kunapendekezwa zaidi kwa ajili ya kudumisha mwili wenye afya njema, kwani kuna mwelekeo wa dhahiri kwamba wakati huo mtu hatakuwa na tumbo lililojaa.

2. Kadhalika, kujamiiana wakati wowote ule ukiwa na tumbo lililojaa ni kwenye madhara. Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba: “Mambo matatu huharibu mwili wa mtu, nayo haya ni pamoja na: kwenda kuoga ukiwa na tumbo lililojaa shibe, kujihusisha na ngono pamoja na mkeo ukiwa na tumbo lililojaa, na kujihusisha na kujamiiana na wanawake wazee, waliodhaifika na wenye umri mkubwa.”70

3. Kuzuia kumwaga manii kwa kurudia mara kwa mara kunaweza kus- ababisha matatizo kwa wanamume, na vile vile hata kwa wanawake.71

Kuimarisha Na Kudhoofisha Tamaa Ya Ngono

Vitu Vinayoongeza Tamaa Ya Ngono:

Vitu Vinayoongeza Tamaa Ya Ngono:72

1. Karoti
2. Vitunguu
3. Nyama
4. Mayai
5. Tikiti maji
6. Komamanga freshi
7. Maziwa halisi
8. Zabibu tamu
9. Mafuta ya ngano

10. Sehemu ya kati ya tende
11. Uvaaji wa viatu vya manjano
12. Kutumia mafuta ya kuchulia kwenye mwili
13. Kupakaza wanja (Kuhl) kwenye macho.

Vitu Vinavyohuisha Na Kuongeza Tamaa Ya Ngono

Vitu Vinavyohuisha Na Kuongeza Tamaa Ya Ngono 73

1. Asali
2. Majozi (walnuts)
3. Tende
4. Ndizi

Vitu Vinavyopunguza Tamaa Ya Ngono

Vitu Vinavyopunguza Tamaa Ya Ngono 74

1. Kuoga kwa kutumia maji baridi
2. Kutokula chakula cha wakati wa usiku

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Kadhim (a.s.): “Kama watu wakiwa na kadiri wakati wa kula vyakula vyao (yaani, wasile kupita kiasi au chini ya kiasi), miili yao wakati wote itakuwa na afya njema; na kamwe msiwache kula chakula cha jioni, hata kama itamaanisha kula vipande vilivyopukuti- ka vya mkate kwa sababu chakula hicho (cha jioni) ni chanzo cha nguvu ya mwili na nguvu ya kujamiiana.75

 • 1. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 23, namba 24927
 • 2. Nikah kwa maneno halisi ina maana ya kujamiiana
 • 3. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 23, namba 24929
 • 4. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 109, namba 25163
 • 5. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 109, namba 25163.
 • 6. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 241, namba 25537
 • 7. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 107, namba 25158
 • 8. Nikah ina maana ya kuingiliana (na mkeo).
 • 9. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 106, namba 25157
 • 10. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk 118, namba 25184
 • 11. Suratun-Nisaa; 4:1, Surat al-Zumar; 39:5, Surat Luqman; 31:28, Suratun-Nahl; 16:72
 • 12. Halliyatul-Muttaqin, Uk. 91
 • 13. Niyaazha wa Rawabith Jinsi wa Zanashui, Uk 38
 • 14. Halliyatul-Muttaqiin, Uk. 110
 • 15. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk.118, namba 25186
 • 16. Halliyatul-Muttaqiin, Uk. 115
 • 17. Ibid., Juz. 20, uk. 188, namba 25185
 • 18. Mustadrak al-Wasaa’il, Juz. 2. Uk.545
 • 19. Niyazha wa Rawabith Jinsii wa Zanashuii, Uk. 55
 • 20. Halliyatul-Muttaqiin, Uk. 111
 • 21. Niyazha wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 52
 • 22. Tib wa Behdaasht, Uk. 200
 • 23. Niyazha wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 24
 • 24. Halliyatul-Muttaqiin Uk. 112.
 • 25. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 144, namba 25258
 • 26. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 134, numba 25253
 • 27. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 147, namba 25266
 • 28. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 148, namba 25271
 • 29. Ibid., Juz. 20, Uk. 120, namba 25190
 • 30. Ibid., Juz. 20, Uk. 137, namba 25238, na uk. 138, namba 25239
 • 31. Niyazha wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 61
 • 32. Wasailush-Shi’a, Juz. 12, Uk. 380, namba 16565
 • 33. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 133, namba 25227
 • 34. Wasailush-Shi’a, Juz. 12, Uk. 382, namba 16568
 • 35. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 134, namba 25229
 • 36. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 132, namba 25222
 • 37. Ibid., Juz. 20, uk. 138, namba 25240
 • 38. Ibid., Juz. 20, Uk. 133, namba 25226
 • 39. Ibid., Juz. 20, Uk. 138, namba 25240
 • 40. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 164, namba 25317
 • 41. Hili limethibitishwa pamoja na ofisi ya Ayatullah Sistanii, Qum
 • 42. Niyaazhaa wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, uk. 71
 • 43. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 21, Uk. 458 namba 27573
 • 44. Niyaazhaa wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii Uk k. 71
 • 45. Niyaazhaa wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 48-49
 • 46. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 2, Uk k. 321, hadith namba 2249
 • 47. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 2 Uk k. 322, hadith namba 2254
 • 48. Halliyatul-Muttaqin, uk. 109
 • 49. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 72
 • 50. Islamic Laws (Shari’ah ya Kiislam) Kanuni namba 520
 • 51. Islamic Laws (Shari’ah ya Kiislam) Kanuni namba 1593
 • 52. Hajj Manaasik, Kanuni ya 219
 • 53. Imethibitishwa na ofisi ya Ayatullah Sistani, Qum.
 • 54. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 257 hadith ya 25570
 • 55. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 109, hadith ya 25164
 • 56. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 54
 • 57. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 126, hadithi ya 25207
 • 58. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 59
 • 59. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 12, Uk. 177, hadithi ya 16008
 • 60. Mengi zaidi hasa yanapatikana kutoka Gonjhaaye Ma’navi, Uk. 318
 • 61. Hili linapendekezwa tu kwenye sehemu ambazo mtu ana uhakika kwamba maji hayo ya mvua hayachafuliwi
  na chochote.
 • 62. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 24-25
 • 63. Halliyatul-Muttaqin, Uk. 172
 • 64. Hii inarejelea kwenye athari za mafuta ya urujuani kwenye joto la tambo/la ndani.
 • 65. Al-Kafi, Juz. 6, Uk. 332
 • 66. Makarim al-Akhlaq, uk.190
 • 67. Biharul-Anwar, Juz. 66, uk. 182, hadithi ya 14
 • 68. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, uk. 22
 • 69. Tib wa Behdaasht, uk. 292
 • 70. Mustadrak al-Wasa’il, Juz. 14, uk. 231 hadithi ya 16578
 • 71. Izdawaaj Maktab Insaan Saazi, Juz. 3, uk. 51
 • 72. Gonjhaaye Ma’navii, uk. 318
 • 73. Tib wa Behdaasht, uk. 300
 • 74. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, uk. 28
 • 75. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, uk. 43