read

Semi Za Imam Ali [a.s.]

*****

Kitabu hiki kilichokuwa mikononi yako ni mkusanyiko ya semi za Amirul Muuminin Ali Bin Abu Talib a.s.
Semi hizi ni mwongozo bora mno kwetu na ime elezwa katika kitabu Ma’anil Akhbaar na Imam Ali ar-Ridha a.s. kuwa, “Kwa hakika, iwapo watu wangelikuwa wamezijua faida na mema ya semi zetu, basi kwa hakika wangelitufuata sisi.” Atakayesoma kitabu hiki ataelewa faida na thamani yake kubwa ya kidini na akizingatia, maisha yake yatakuwa mema sana.

*****

Dibaji

Mtukufu Amirul Muuminin (Bwana wa Waumini) alizaliwa miaka 23 kabla ya Hijriya (sawa na mwaka 599 Miladia) mjini Makka. Mnamo tarehe 21 Ramadhan mwaka 40 Hijria (mwafaka Januari 24, 661 Miladia), wakati wa sala ya asubuhi, aliuawa shahidi na Abdul Rahman ibn Muljim Muradi katika mji wa Kufa na akazikwa katika mji wa Najaf ulio karibu na Kufa (Iraq).

Imam Ali (a.s.) ni mkwe wa Mtume Muhammad (s.a.w.) na ni mmojawapo kati ya watu wenye hekima kubwa kabisa katika Uislamu. Si kwamba alikuwa amiri mkubwa na msambazaji halisi wa Uislamu tu, bali kwa wakati huohuo alitawala daraja za juu kabisa katika fani za hekima, bayani na fasihi, na alikuwa ni miongoni mwa Maimamu wa Waislamu.

Ali bin Abu Talib (a.s.) alikuwa msemaji fasihi sana kwa kadiri kwamba semi na khutba (hotuba) zake zina thamani kubwa sana. Miongoni mwa athari zake nyingi zilizobakia ni kitabu kiitwacho Nahjul Balagha (Njia ya Balagha) ambacho bado ni kipya ingawa zimekwishapita karne 13 tangu azitoe lulu na johari hizo.

Nahjul Balagha imekusanywa na Sayyid Radhii ambaye alikuwa mmojawapo kati ya wanavyuoni wakubwa wa Kiislamu. Ilivyokuwa kusoma na kutalii kitabu chote hicho kunahitaji wakati mwingi, na kukichunguza kipawa chote hicho cha Kiislamu si jambo linaloweza kufanywa na kila mtu, hivyo, watafiti na wachunguzi wengi wamezichagua nasaha na semi za Mtukufu huyo na kuziandika. Maandiko hayo wameyaita: Methali (semi fupi) au Nasaha Murua. Hapana shaka kwamba kitabu hiki kidogo ni kama kitone kimoja cha maji ya bahari kilichodondoshwa ili tufaidike nacho.

Haiwezekani kuhifadhi kikamilifu utamu na ufasaha wa maudhui ya asili ya lugha moja wakati unapoitafisiri kwa lugha nyingine; na kwa sababu hii, tunaweza kusema kwamba wataalamu wa lugha ya Kiarabu ndio wanaoweza kufahamu na kupata ladha zaidi ya utamu na ufasaha uliomo katika maneno ya hekima ya Imam Ali (a.s.). Tarjumi hii ya Kiswahili imefanywa na rafiki yangu mpenzi Ndugu Muhammad Ridha Shushtary.

Wale watu wenye busara na maarifa wamebainisha ukweli huu kwamba maneno murua na nasaha za hekima zilizokusanywa katika kitabu hiki kwa ajili ya wasomaji watukufu zina thamani kubwa na ukweli wa daima.

Dk. Mir Mahmoud Daawati
Machi 24,1986
Rajab 13, 1406

(1) Mwenyezi Mungu

Mche Mwenyezi Mungu ambaye husikia msemapo na hujua mwazapo.
Ikiwa mwampenda Mwenyezi Mungu, toeni mapenzi ya dunia nyoyoni mwenu.
Sikuhimizini kumtii Mwenyezi Mungu ila kwamba nimekutangulieni kumtii Yeye; wala sikukatazeni maasia ila kwamba kabla yake nimejikataza mwenyewe.
Amebarikiwa yule afufuaye haki, auaye batili, apingaye udhalimu na aimarishaye uadilifu.
Amebarikiwa yule adhibitaye matamanio ya nafsi yake ili asimwasi Mwenyezi Mungu.
Ajuaye nafsi yake amjua Mola wake.
Sikumkana Mwenyezi Mungu tangu nimjue.
Sikumshuku Mwenyezi Mungu tangu nimwone.
Ewe Mola wangu! Ukubwa uoje wa uumbaji Wako tuuonao, lakini udogo uoje ukilinganishwa na kudura Zako tusizoziona.
Haihata! Lau si kumcha Mungu ningelikuwa mjanja kuliko Waarabu wote.
Utukufu hupatikana kwa kumtumikia Muumba; na mwenye kuutafuta kwa viumbe hatoupata.
Kumcha Mwenyezi Mungu huleta amani.

(2) Dunia

Dunia ni kivuli cha mawingu, na ndoto ya usin­gizi: furaha hufuatana na ghamu, na asali huchanganyika na sumu.
Dunia ni kama nyoka: mguso wake ni mlaini na sumu yake huua.
Dunia ni makazi yaliyozungukwa na balaa na yaliyopambwa kwa udanganyifu: hazidumu hali zake wala hawasalimiki wakazi wake.
Dunia ni nyumba iliyo duni mbele ya Mola wake, hivyo, ikachanganywa halali kwa haramu yake, mema kwa maovu yake, na matamu kwa machungu yake.
Ukamilifu haupo duniani.
Ewe dunia! Mdanganye mwingine. Sina haja nawe; nimekutaliki mara tatu na sitokurejea tena.
Itazame dunia kwa mtazamo wa mtawa aliyejitenga, na wala usiitazame kwa mtazamo wa ashiki aliyeikufia.
Hakika dunia yenu machoni mwangu ni duni zaidi kuliko utumbo wa nguruwe ulio mkononi mwa mwenye ukoma, na ni hafifu zaidi kuliko jani lililo mdomoni mwa panzi.
Hakika ndani ya ardhi imekufa, na nje yake ina­umwa.
Wakazi wa dunia ni mbwa wabwekao na wanyama wa mwitu wangurumianao. Wenye nguvu huwala walio dhaifu, na wakubwa huwagandamiza wadogo. Ni kama mifugo, wengine wamefungwa na wengine hawakufungwa.

(3) Binadamu

Ajabu ioje binadamu huyu! Huona kwa shahamu, husema kwa nyama, husikia kwa mfupa, na huvuta pumzi kupitia tundu!
Malaika wa Mwenyezi Mungu hunadi kila siku:
“Enyi watu wa duniani! Zaeni kwa ajili ya mauti, kusanyeni mali kwa ajili ya maangamizo, na jengeni kwa ajili ya mabomoko."
Vipi binadamu hujivuna? Mwanzo wake ni manii na mwisho wake ni mzoga; hawezi kujilisha mwenyewe wala hawezi kujikinga na mauti.
Maskini binadamu! Hajui ajali (mauti) yake, hafahamu ugonjwa wake, huhifadhi vitendo vyake, mbu humuuma, kupalia humuua, na jasho humnukisha.

(4) Maisha

Kumbuka kila starehe ina mwisho wake, na kila neema ina kupita (kutodumu) kwake.
Siku zako zilizopita zimekwishapita, na zilizo­bakia hazijulikani; hivyo, chukua fursa ya wakati wako kwa kufanya kazi.
Maisha ni adui usiyemfanyia uadui, na dhalimu usiyemdhulumu, na mchokozi usiyemchokoza.
Ni ujinga kujivunia yale yasiyobaki kwa ajili yako wala wewe hubaki kwa ajili ya hayo.
Matunda ya maisha marefu ni maradhi na ukongwe.
Vitu vitatu havipatani na maisha ya mtu: chuki, uhasidi na tabia mbaya.
Vitu vitatu ni miongoni mwa balaa (mtihani) kubwa: familia (aila) kubwa, deni kubwa, na maradhi yanayoendelea.
Saa moja ya madhila haiwi sawa na maisha yote ya utukufu.
Thamani ya mtu hujulikana katika mabadiliko ya maisha.
Kila lililopita ni kama halikuwepo, na lijalo ni kama lipo.
Vipi wafurahia umri (maisha) ambao kila saa wapungua?
Hakuna mtu apataye furaha duniani bila ya kutokwa na machozi baadaye.
Aishiye sana atahuzunishwa na vifo vya marafiki zake.
Kuingiliana na watu duni (visirani) ni alama ya bahati mbaya.
Haraka ioje saa kuwa siku, na siku kuwa mwezi, na mwezi kuwa mwaka, na miaka kumaliza umri!
Dunia ni kama kivuli chako: ukisimama husi­mama, na ukikifuatia hukukimbia.
Urafiki wa dunia ni shabaha ya mageuko na bahati mbaya.
Dunia (maisha) ni sumu hunywiwa na asiyeijua.
Mabadiliko hutengenea yatokeapo, (lakini) dunia huvunjika iungwapo.
Dunia imkubaliapo mtu humpa mema ya wengine, na imgeukiapo mtu humnyang'anya mema yake.
Wako wapi wale waliokuwa na umri mrefu kuliko nyinyi na kumbukumbu kubwa kabisa? Wako wapi wale waliojenga na kurefusha (majumba), waliotia samani (fanicha) na kupamba, waliokusanya (hazina) na kuhesabu? Wako wapi Kisra, Kaizari, Tubba na Himyar?
Utamu wa maisha ni kukataa madaha (mbwe­mbwe).
Dunia na Akhera ni kama mume mwenye wake wawili: mmoja ukimridhisha, mwingine huudhika.

(5) Mauti

Namstaajabia asahauaye mauti wakati amwona afaye.
Kila chenye uhai hufa, na kila kitu (kisichokuwa na uhai) huangamia.
Asiyenufaisha maisha yake, basi ahesabiwe katika waliokufa.
Aishiye hufa.
Ategemeaye kufa aharakishe kufanya mema.
Kila pumzi moja ya mtu ni hatua moja kufikia mauti yake.
Nyinyi mwawindwa na mauti ambayo mkisimama yatakukamateni, na mkikimbia yatakuwahini.
Kifo cha mwana huvunja kiuno.
Kifo bora kabisa ni kuuawa (katika medani). Naapa kwa Aliye na roho yangu mkononi Mwake kwamba ni afadhali kufa kwa dharuba elfu za upanga kuliko kufa kitandani.

(6) Mtu Mwema

Mtu mwema ni hai hata kama atahamishwa katika makazi ya wafu.
Mtu mwema hugombana akitendewa vibaya, lakini huonyesha upole akitendewa vyema. Mshari hugombana akitendewa vyema, na halainiki mpaka atendewe vibaya.
Watu ni kama miti: maji yake ni mamoja na matunda yake ni tofauti.
Watu wastahikio zaidi rehema ni: aalimu (msomi) aamuruwaye na jahili, karimu aamrishwaye na bakhili, na mwema atawaliwaye na mwovu.
Mtu bora kabisa ni yule awafaaye zaidi watu.
Watambuao fadhila (wema) za wafadhili ndio wenye fadhila.
Mheshimiwa haringii cheo alichokipata hata kama ni kikubwa kama mlima usiotikisika kwa upepo; na mtu duni hubabaishwa na cheo kidogo kama majani yapeperu­shwayo na upepo.
Mara ngapi mtu alaumiwa wakati hana kosa.
Miongoni mwa matendo bora ya mtu mwema ni kutojali aibu azijuazo za wengine.
Miongoni mwa masaibu makubwa ya watu wema ni kuwa na haja ya kuwanyenyekea watu waovu.
Watu wamelala, wataamka watakapokufa.
Uungwana ni jina (neno) likusanyalo sifa na mema yote.

(7) Mtu Mwovu

Mwenye ubinafsi haoni aibu zake, na kama aki­ona uzuri wa mwenziwe, dosari na aibu zake zitamchusha.
Mwovu hayawazii mema ya mtu yeyote kwa sababu haoni kitu ila kwa mujibu wa umbile la nafsi yake.
Watu wachukiwawo sana na Mwenyezi Mungu ni:
maskini ajionaye, mzee mzinifu, na mwanachuoni mwovu.
Mtu mwovu kuliko wote ni mwenye kujiona kwamba yeye ni bora kuliko watu wote.
Mtu mwovu kuliko wote ni yule asiyejali kwamba watu wamwona mwovu.
Mtu mwovu kuliko wote ni yule atafutaye aibu za watu na zake mwenyewe hazioni.
Mtu mwovu kuliko wote ni yule alipaye baya kwa zuri (alilofanyiwa); na mtu mwema kuliko wote ni yule alipaye zuri kwa baya (alilofanyiwa).
Wakimbieni kwa mbio zote mwovu na fasiki.
Kuwafanyia ubaya watu wema ni alama moja ya ubaya.

(8) Uchaji

Ucha Mungu (takwa) ni ufunguo wa ufanisi.
Nguo ya takwa (uchaji) ni vazi bora kabisa.
Ucha Mungu ni dalili ya imani (dini).
Kilele cha ucha Mungu ni kuacha matamanio.
Usafi (wa moyo) hudhoofisha matamanio.

(9) Aibu

Wenye aibu hupenda kutangaza aibu za watu wengine ili wapate kisingizio cha kuwafedhehi.
Mojawapo kati ya alama za mjinga ni kubadilisha sana mawazo yake.
Aibu zako husitirika hadhi yako ikibahatika.
Aibu kubwa kabisa ni kutoa aibu ya mwingine ambayo wewe pia unayo.

(10) Mafunzo

Vitabu ni mabustani ya wanavyuoni.
Mwanachuoni (aalimu) yu hai hata kama amekufa.
Mwanachuoni ni yule afahamuye kwamba yale ayajuayo ni machache kuliko yale asiyoyajua.
Akubaliaye maoni mazuri hujua mahali palipo na makosa.
Tumaini ni kama sarabi, humdanganya mwenye kuiona na humvunja moyo mwenye kuitumainia.
Asiyejifunza hatofunzwa.

(11) Elimu

Mali hupungua kwa kuitumia, na elimu huzidi kwa kuitumia.
Elimu hukuokoa, ujinga hukutupa.
Mtu ni adui wa asiyoyajua.
Elimu haimaliziki.
Elimu ni hazina kubwa isiyomalizika; akili ni nguo mpya isiyochakaa.
Elimu huongoza kwenye akili, hivyo, aliye­elimika ameerevuka.
Tafuteni elimu mjulikane kwayo, na itekelezeni muwe wanavyuoni.
Tafuteni elimu ikupatieni hadhi.
Mwenye elimu kuliko watu wote ni yule ambaye yakini yake haibabaishwi na shaka.
Sumu (maafa) ya elimu ni kutoitumia: sumu ya kitendo (amali) ni kutokuwa na ikhlasi nacho.
Chukua kutoka kila elimu kilicho bora yake, kwani nyuki hunywa kutoka kila ua kilicho kizuri chake.
Asili ya utukufu ni elimu.
Kuanguka kwa elimu ni kama kuvunjika kwa chombo ambacho huzama na kuwazamisha waliomo.
Vitu viwili haviwezi kufikiwa mwisho wake:
elimu na akili.
Kila kitu huwa na thamani kinapokuwa adimu, isipokuwa elimu ambayo huwa na thamani zaidi kila inapo­tolewa kwa wingi.
Vipi mtu amjue mwingine asipojijua mwenyewe?
Afichaye elimu atakuwa mjinga.
Akosaye uzoefu hudanganywa.
Asione haya mtu kusema, "Sijui!" aulizwapo jambo asilolijua.
Msiyachukie yale msiyoyajua, kwani sehemu kubwa ya elimu ni katika yale msiyoyajua.
Hakuna hazina bora kama elimu.
Utukufu wa mtawala upo katika utawala wake, na wa mwanachuoni katika elimu yake, na wa tajiri katika utajiri wake, na wa mzee katika umri wake.
Chuma elimu, kwani hukupamba ukiwa tajiri, na hukulisha ukiwa maskini.
Nguo ya elimu hukudumisha daima na haichakai, na hukuendeleza bila ya kuraruka.
Elimu ifaayo zaidi ni ile itendwayo.
Uzoefu ni elimu iliyotumiwa.
Mwenye elimu humjua mjinga kwa kuwa zamani mwenyewe alikuwa mjinga, lakini mjinga hamjui mwenye elimu kwa kuwa kabla yake hakuwa mwenye elimu.

(12) Mafundisho

Mwalimu na mwanafunzi ni washiriki wawili wapatao thawabu.
Mwenye elimu hutazama kwa mtazamo wa moyo wake, lakini mjinga hutazama kwa mtazamo wa macho yake.
Sikiliza ujifunze, na kaa kimya usalimike.
Mtu dhaifu kabisa kuliko wote ni yule asiyeweza kujirekebisha mwenyewe.
Adabu njema huficha nasaba mbaya.
Elimu isiyokujenga ni upotovu.
Asiyeweza kujirekebisha nafsi yake, hawezi kumrekebisha mtu mwingine.
Asiyeweza kustahamili taabu ya kujifunza, atabaki katika madhila ya ujinga.
Aulizaye hujifunza.
Elimu bora kabisa ni ile ikutengenezayo.
Mwenye kuabudu bila ya kuwa na elimu ni kama punda anayezungusha kijaa bila ya kutoka nje ya mahali pake.
Ukimwona mwanachuoni, kuwa mtumishi wake.
Nyinyi mwahitajia zaidi kupata mafunzo mazuri kuliko fedha na dhahabu.

(13) Hekima

Mwenye akili hutegemea kazi (matendo yake); mjinga hutegemea tumaini lake.
Hekima ni mti uotao katika moyo na utoao matunda katika ulimi.
Kumtumainia kila mtu kabla ya kumjaribu ni kukosa akili.
Akili ikikamilika, matamanio hupungua.
Mafanikio ya mambo yote hupatikana kwa kutumia akili.
Dhana ya mwenye akili yasihi zaidi kuliko uha­kika wa mjinga.
Mwenye akili hutafuta ukamilifu; mjinga hutafuta mali.
Ni busara kumtii mkubwa wako, kumheshimu aliye sawa nawe, na kuwafanyia insafu wadogo wako.
Hakutoa Mwenyezi Mungu kati ya waja Wake kitu kilicho bora zaidi kuliko akili.
Yafaa kwa mwenye akili kila siku aweke saa moja asiyokuwa na kazi kujichungua nafsi yake kwamba ame­chuma nini na amepoteza nini.
Moyo ni chemchemi ya hekima, na sikio ni mfe­reji wake.
Imani na akili ni ndugu pacha; hakubaliwi mmoja­wapo bila ya mwenziwe.
Hakika mtu aliye makini haathiriki na hadaa (ya wengine), wala mwenye akili hahadaiki na tamaa.

(14) Akili

Mwerevu ni yule ambaye leo yake ni bora kuliko jana yake.
Upofu wa jicho ni bora kuliko upofu wa busara.
Binadamu ana vitu viwili vilivyo bora: akili na mantiki. Hujinufaisha mwenyewe kwa akili, na huwanufa­isha wengine kwa mantiki.
Afanyaye usuhuba na wenye akili atapata heshima.
Mwenye kuwa na fahamu hatakuwa fakiri kabisa.
Akili ni umbile, huzidi kwa elimu na uzoefu.

(15) Tafakuri

Mambo yasiyofahamika hufahamika kwa kufikiri.
Fikra za mtu ni kama kioo, humwonyesha vitendo vyake vyema na viovu.
Fikiri kisha useme, ili usalimike na upotevu.
Kila aliye na tafakuri hupata mzingatio kutoka kila kitu.
Mwenye kutafakari juu ya neema za Mwenyezi Mungu atafuzu.
Ukitanguliza fikra katika vitendo vyako, matokeo yake yatakuwa mema katika kila jambo.
Zingatia kabla ya kuhujumu.

(16) Ujinga Na Upumbavu

Upumbavu ni ugonjwa usio na dawa na maradhi yasiyopona.
Ujinga ni adui mbaya sana.
Jahili hatambui kosa lake, wala hakubali nasaha ya mtu.
Ujinga ni mwamba usiobubujika maji humo, na ni mti wenye matawi yasiyochipua majani, na ni ardhi isiyoota mimea.
Mtu mpumbavu kabisa ni yule anayedhani kwa­mba ni mtu mwenye akili kuliko wote.
Kati ya alama za mpumbavu ni kubadilisha sana mawazo yake.
Ujinga kwa mwanadamu una madhara zaidi kuliko kidonda katika mwili.

(17) Usemi

Ulimi ni mnyama awindaye, ukimwacha ataku­uma.
Ufasaha ni kurahisisha usemi, na kufanya kuwa mwepesi kwa akili (fahamu).
Moyo ni hazina ya ulimi, na ulimi ni mkalimani wa mtu.
Usemi ni kama dawa: kidogo ni nafuu, nyingi ni madhara.
Jihadhari na usemi wa jambo usilolijua mwendo wake wala ukweli wake, kwani usemi wako huonyesha akili yako, na maneno yako hudhihirisha maarifa yako.
Jihadhari na ulimi wako, kwani ni mshale unao­kosa shabaha.
Usemi bora kabisa ni ule unaoambatana na matendo.
Usemi bora kabisa ni ule usioyakera masikio, wala usioitaabisha akili kufahamu.
Usemi ukikubaliana na nia ya msemi, hukubaliwa na msikilizaji, na ukienda kinyume na nia yake, hautasi­mama mahali pake.
Ikiwa wewe si msemaji mwenye elimu, basi kuwa msikilizaji msikivu.
Maradhi ya usemi ni kusema sana.
Semeni mjulikane, kwani mtu amejificha chini ya ulimi wake.
Mtu mpumbavu hutambulikana kwa njia tatu:
huzungumzia asilolijua, hujibu asiloulizwa, na hufanya mambo bila ya kuzingatia.
Maneno mengi ni makali kama ncha ya upanga.
Mara nyingi mapigano husababishwa na tamko moja tu; mara nyingi mapenzi makubwa yametokana kwa kutupa jicho tu.
Mara nyingi maneno huchoma zaidi kuliko mishale.
Kuteleza kwa hatua huumiza, kuteleza kwa ulimi huua.
Usikiaji wa sikio haufai ukiwa pamoja na usahaulivu wa moyo.
Watu wangapi wameangamizwa na ndimi zao wenyewe.
Kusema sana huchokesha baraza.
Mpumbavu hula kiapo kwa kila kauli.
Ulimi wa mjinga ni ufunguo wa mauti yake.
Asemaye yasiyofaa, atasikia asiyoyapenda.
Mwenye kusadikisha usemi wake, huimarisha hoja yake.
Asemaye kweli katika usemi wake, huzidisha utukufu wake.
Mwenye kutosheka (kusema kwa) kuashiria, hata­ hitajia kusema waziwazi.
Lau mtu asingekuwa na ulimi (usemi), asingekuwa kitu ila ni taswira iliyochorwa au mnyama asiyefaa.
Usitazame ni nani anayesema, bali tazama ni nini linalosemwa.
Usiyadharau maoni ya thamani hata yakitoka kwa mtu duni.
Usiseme usipopata wakati ufaao wa kusema.
Hifadhi kichwa chako kutokana na kuteleza ulimi wako.
Hati ni mkono wa ulimi.
Jihadhari na kusema sana, kwani huzidisha ma­kosa na huleta uchofu.
Ncha ya ulimi ni mkali zaidi kutiko ncha ya mkuki.

(18) Kusingizia Na Kusengenya

Mkane mwambi na msingiziaji, hata kama (ma­neno yake) ni uwongo au kweli.
Jihadhari na sakubimbi, kwani hupanda mbegu ya chuki na hukuweka mbali na Mwenyezi Mungu na watu.
Asikilizaye watu wakisemwa, naye pia ni msenge­nyaji.
Jihadhari na maneno yasiyofaa, kwani hutia hamaki nyoyoni.

(19) Ukweli

Ukweli ni njia nyoofu kabisa; elimu ni mwongozo bora kabisa.
Ukweli ni dawa ya uwokovu.
Piganishaneni maoni mbalimbali ili ukweli uto­keze.
Kuweni wakweli katika maneno yenu na wanyofu katika matendo yenu.
Maneno hupambika kwa ukweli.
Ukweli bora kabisa ni kutekeleza ahadi.

(20) Uwongo

Kumfanyia ujanja akuaminiaye ni kukufuru.
Uwongo ni hiana.
Msema kweli ni mahashumu na mtukufu; mwongo ni mtu duni na dhalili.
Hila hurudufu madhambi.
Jizuie kuingiliana na mwongo; na ikibidi kuingili­ana naye, usimsadiki wala usimfanye ajue kwamba wajua asema uwongo, kwa sababu ataacha urafiki nawe lakini hatoacha tabia yake.
Ukweli umepungua kati ya watu, na uwongo ume­zidi; ndimi zazungumzia urafiki lakini nyoyo zimejaa uadui.
Ukweli kidogo huondosha ubatilifu mwingi, kama vile moto mdogo uunguzavyo kuni nyingi.
Ajulikanaye kwa kusema uwongo hupungua kuaminiwa kwake.
Kuwa bubu ni afadhali kuliko kusema uwongo.

(21) Ukimya

Ukimya hukuvisha nguo ya utulivu na hukukinga na haja ya kutoa visingizio.
Ukimya bila ya kutafakari ni ubumbuazi.
Usemaji usifikanao sana ni kukaa kimya wakati usipotakikana kusema.
Ukimya huzidisha makini.
Mara nyingi ukimya ni jawabu ya swali.
Ukimya wa mjinga ni kificho chake.
Si katika tabia za Mitume kujisifu mno.
Ukimya ni bustani la tafakari.
Jiepushe na kujisifu mno, kwani majisifu si katika sifa za imani.
Jawabu fasihi kabisa kwa mpumbavu ni kuto­mjibu.

(22) Siri

Siri ya mwenye hekima ni hazina ya ajabu.
Ameridhika na madhila yule afichuaye siri zake kwa wengine.
Asiyeweza kuficha siri zake hawezi kuficha siri za wengine.

(23) Unafiki

Ulimi wa mnafiki ni mtamu, lakini moyo wake ni mchungu.
Watu wanafiki hujipamba kwa uwongo.
Ulimi wa mnafiki ni mzuri, lakini moyo wake una maradhi.
Akufichuliaye siri zako hukuharibia mambo yako.
Achukiza sana mtu mwenye nyuso mbili.

(24) Kusifu

Jihadharini na kujisifu na kujitukuza sana, kwani hutoa harufu mbaya katika moyo.
Jihadhari na kumsifu mtu kwa jambo asilokuwa nalo, kwani kitendo chake huthibitisha sifa yake na hukuka­dhibisha wewe.
Ukweli unaochukiza kabisa ni mtu kujisifu mwenyewe.
Akusifuaye kwa jambo usilonalo, itambidi aku­laumu kwa jambo usilonalo.
Ajitukuzaye mwenyewe hujidhalilisha.
Miongoni mwa mambo yachukizayo mno ni kuwasifu watu duni.
Kumsifu mtu kwa jambo asilokuwa nalo ni kumstihizai.
Kuwasifu waovu ni katika madhambi makubwa sana.

(25) Mzaha Na Kucheka

Mzaha huleta chuki.
Kucheka sana huondoa heshima.
Afanyaye mzaha sana hazingatiwi.
Jiepushe na kusema maneno ya kuchekesha hata kama wahadithia kutoka kwa mwingine.

(26) Ufidhuli

Amtoleaye ufidhuli mfalme hujitakia madhila.
Kukosa haya humfedhehesha mtu.
Uso mbaya kabisa ni wa fedhuli.

(27) Nasaha

Asikilizaye nasaha huepukana na makosa; asiye­shauriana na watu hujitia katika makosa.
Mhubiri asiye na amali ni kama upinde usio na mshale.
Chukua ushauri wa adui wako aliye na akili, na jihadhari na rai ya rafiki yako mjinga.
Shauriana na maadui zako ujue rai zao, kiwango cha uadui wao na msimamo wa makusudio yao.
Mtu bora kabisa katika (kutoa) maoni ni yule asiyekataa ushauri.
Mnasihi bora kabisa kwako ni dunia ikiwa utasiki­liza nasaha.
Shauriana na wenye akili usalimike na lawama na majuto.
Akuuziaye nasaha hukupatia faida.
Kumnasihi mtu mbele ya watu ni kumlaumu.
Jiongozeni kwa taa ya waadhi wa mwenye ku­tenda ayasemayo.
Hakika tumehimizwa kutaka ushauri, kwani rai ya mshauri ni safi, na rai ya mshauriwa ni mseto.

(28) Upweke

Asiyewahitajia watu, Mwenyezi Mungu atamto­sheleza.
Awajuaye watu hatawatumainia.
Ajitengaye husalimika.
Awajuaye watu hujitenga nao.
Aijuaye dunia ataiachilia mbali.
Afadhali mtu kuwa peke yake kuliko kuwa na rafiki mwovu.

(29) Kutoa

Mpe mhitaji kabla hajakuomba, kwani ukimfanya akuombe kitu utakuwa umemwondoshea heshima yake ambayo ni bora zaidi kuliko kile umpacho.
Nyinyi mnahitajia zaidi kutoa katika yale mliyo­yachuma kuliko kuchuma mnayoyachuma sasa.
Uchangamfu hupendeza wakati wa kutoa (uka­rimu).
Ubora wa ukarimu ni kutoa kwa haraka.
Asiye na dini hana murua.
Aliyebarikiwa neema nyingi na Mwenyezi Mungu, atazidiwa na watu wenye kumhitajia; hivyo, ikiwa atateke­leza kama vile alivyoamuriwa na Mwenyezi Mungu, neema hizo zitadumu, lakini akizuia kutekeleza, atapoteza aliyo­neemewa.
Akataaye kutoa hujikatalia sifa.
Mwenye kumpa usalama mwoga, Mwenyezi Mungu atamsalimisha na adhabu Yake.
Ni murua kamili kusahau haki yako na kukum­buka haki ya wengine juu yako.
Ni katika murua mtu kuhiari kutoa mali yake ili kuhifadhi heshima yake.
Mojawapo kati ya ukarimu bora kabisa ni mtu kuwakirimu wageni hata kama ni kwa kujitwika gharama (za madeni).
Usiakhirishe kumkidhia haja mhitaji mpaka kesho, kwani hujui litakalokufikieni.
Usione haya kutoa kidogo, kwani kunyima ni kidogo zaidi.
Watu ni wa aina mbili: mkarimu asiyetajirika, na tajiri asiyetoa.
Ukarimu bora kabisa ni kutoa haki kwa wanao­stahiki.
Hakika utoaji (ukarimu) wa Mwenyezi Mungu haupingani na hekima Yake, hivyo, hajibu kila ombi analo­ombwa.
Nguo utakayomvisha mwingine itakupa faida zaidi kuliko ukiivaa mwenyewe.

(30) Hisani Na Wema

Ihsani humtia mtu utumwani; masimango huha­ribu ihsani.
Ukimfanyia mtu mema ficha, (lakini) ukifanyiwa mema tangaza.
Kufanya wema humtia mwungwana utumwani.
Kuwa mwenye kuamrisha mema na kukataza maovu.
Usimfanyie shari akufanyiaye hisani; na mwenye kumfanyia shari yule aliyemfanyia hisani huzuia watu wasi­fanye mema.
Kumfanyia mema yule asiyestahiki ni kuuharibu wema.
Wasiwe sawa mbele yako mwema na mwovu, kwani huko ni kumfanya mwema kuacha kufanya wema, na mwovu kuendelea na uovu.
Kuwa mpole ni kujipunguzia shida.

(31) Israfu

Majivuno ni sawa na upumbavu; ubadhirifu ni alama ya uhitaji.
Matumizi mazuri huzidisha mali iliyo kidogo, na matumizi mabaya hupoteza mali iliyo nyingi.
Acha ufujaji, kwani mfujaji hasifiwi kwa ukarimu wake, wala hapewi pole kwa umaskini wake.
Kuwa mkarimu lakini usiwe mbadhirifu.

(32) Jazaa

Apandaye mti wa mema, atachuma matunda matamu sana.
Mtu huvuna alichopanda, na hulipwa alilofanya.
Apandaye mema atapata tunzo yake.

(33) Siasa

Siasa nzuri huimarisha (hudumisha) uongozi.
Ni lazima kwa mtawala kujitawala mwenyewe kabla ya kuwatawala raia zake.
Utawala wa watu duni ni madhila kwa watukufu.
Utawala huanguka kwa kuja madarakani walio duni.
Mtawala mwovu kabisa ni yule aogopwaye na watu wanyofu.
Nchi mbaya kabisa ni ile ambayo raia zake hawana usalama.
Mwenye kuwa na udhaifu katika siasa (uende­shaji), atadharauliwa katika uongozi.
Ni wajibu kwa mtawala kuwatakia raia zake yale ajitakiayo mwenyewe.
Vitu vinne ni dalili ya kuanguka serikali: kuacha misingi, kushikilia mambo madogo, kuja juu walio duni, na kuanguka walio bora.
Siasa ngumu sana ni kubadilisha desturi.

(34) Uadilifu

Haki ni upanga usoingia butu.
Uadilifu ni nguzo ya raia.
Fanya uadilifu nguvu zako zidumu.
Maradhi ya umma ni mwanachuoni fasidi; maradhi ya uadilifu ni mtawala dhalimu.
Zaka ya mtawala ni kuwasaidia wenye mashaka.
Zaka ya madaraka ni insafu.
Mwenye kuwa mwadilifu katika utawala (uongozi) wake hahitajii wenzake.
Hakuna kitu kihifadhicho serikali kama uadilifu.
Kati ya daawa mbili zikinzanazo mojawapo si kweli.

(35) Dhuluma

Uadilifu mzuri kabisa ni kumsaidia mdhulumiwa.
Watu wa aina tatu hawatatazamwa na Mwenyezi Mungu: mwenye kudhulumu; mwenye kumsaidia dhalimu; na mwenye kuridhia udhalimu.
Mtawala bora kabisa ni yule aondoshaye udhalimu na afufuaye uadilifu.
Mnyama mkali mla watu ni bora kuliko mtawala dhalimu katili.
Asaidiaye ubatilifu hudhulumu haki.
Adhulumiaye katika utawala wake, watu (wake) wataomba mauti yake.
Mwenye kujionea huruma mwenyewe, hatam­dhulumu mwingine.
Mwenye kudhulumu atadhulumiwa.
Mojawapo kati ya uhalifu mkubwa sana ni kuha­ribu sanaa.
Ni rahisi mtu kuvumilia kifo cha mwanawe kuliko kuvumilia udhalimu.
Siku ya mdhulumiwa kulipiza kisasi kwa dhalimu ni ngumu zaidi kuliko siku ya dhalimu kumdhulumu mdhu­lumiwa.
Jihadhari na udhalimu, kwani dhalimu hatosikia harufu ya Pepo.
Jihadhari na kumdhulumu mtu asiye na msaidizi mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Ukimwona mdhulumiwa, msaidie dhidi ya dhalimu.

(36) Kudhulumu

Udhalimu huharibu nchi.
Kudhulumu hufuatiwa na maangamizo.
Mwenye kushika hatamu za udhalimu, atatupwa na farasi wake.
Mawaziri waovu ni wasaidizi wa madhalimu na ndugu wa watendao dhambi.

(37) Ujamaa

Wakirimu jamaa zako. Waheshimu werevu wao na wavumilie wapumbavu wao. Na wasaidie wenye shida kati yao, kwani wao watakuwa ni msaada mkubwa kwako wakati wa faraja na dhiki.
Mara nyingi jamaa huwa mbali kuliko mtu baki.
Uhasama kati ya jamaa huchoma zaidi kuliko sumu ya nge.

(38) Urafiki

Urafiki humfanya mtu baki kuwa jamaa.
Urafiki ni ujamaa ulio karibu kabisa.
Ndugu yako hasa ni yule akusaidiaye wakati wa shida.
Bashasha huvuta urafiki.
Mgeni ni yule asiye na rafiki.
Marafiki ni nafsi moja katika viwiliwili tofauti.
Mfanyie rafiki yako kila aina ya mapenzi, lakini usimpe siri yako.
Rafiki akikufanyia hiana ni rahisi kumuacha.
Uzuri wa kila kitu ni upya wake, na rafiki bora kabisa ni wa zamani zaidi kushinda wengine.
Mara nyingi rafiki hukudhuru kutokana na ujinga wake na wala si kwa kukusudia.
Mara nyingi uhusiano (wa kirafiki) huwa ni afadhali zaidi kuliko uhasama wa kijamaa.
Marafiki zako walio wabaya kabisa ni wale waku­sifiao mno na wasiokuambia makosa yako.
Marafiki wabaya ni wale wakugandao wakati wa faraji na wakuachao wakati wa dhiki.
Wakati wa kupungua neema hubainika kati ya rafiki na adui.
Si rafiki yako yule akufanyaye utake mwamuzi aamue kati yenu.
Lau dunia nzima akipewa mnafiki ili anipende, hatanipenda.
Awachaye marafiki kutokana na kila kosa dogo, atakosa marafiki.
Mwenye kukufuata wakati wa ufanisi wako ataku­acha wakati wako wa mashaka.
Mwenye kuwa na dhana nzuri juu ya watu, ata­pata mapenzi yao.
Apendaye kitu hukitaja kila mara na hukisifu.
Usimfanye rafiki yako adui wa rafiki yako.
Usiende kinyume na haki ya rafiki yako kwa sababu ya urafiki baina yenu, kwani hawezi kuwa rafiki yako zisipoheshimiwa haki zake.
Usifanye urafiki na watu wengi wa dunia, kwani ukishindwa kuendeana nao watakuwa maadui zako. Mfano wao ni kama moto, wengi wao watakuunguza na wachache watakunufaisha.
Jihadhari na urafiki wa mpumbavu, kwani akitaka kukunufaisha hukudhuru.

(39) Maadui

Adui mmoja ni sawa na wengi.
Asiyeweza kupambanua jema kutoka katika ovu ni mnyama.
Awaachaye marafiki zake, huwasaidia maadui zake.
Mwenye kudhoofika bahati yake, huimarika wapinzani wake.
Usimdharau adui hata akiwa dhaifu.
Usidanganyike na mwendo mzuri wa adui, kwani amefanana na maji ambayo licha ya kupashwa moto kwa muda hayatozuia kuuzima.
Adui duni kabisa na mwenye chuki ni yule adhihirishaye uadui wake.
Likitokea baina yako na adui wako suala la kufun­giana mkataba wa suluhu na ukawajibika kutekeleza, basi heshimu ahadi yako kwa kutimiza, na tekeleza dhima yako kwa uaminifu.

(40) Ushujaa Na Woga

Mwoga hana maisha (ya raha).
Oneni haya kukimbia (vitani), kwani ni fedheha kwa vizazi vyenu, na kuna (malipo ya) Moto katika Siku ya Hesabu.
Zaka ya ushujaa ni kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Lau vitu (viovu na vizuri) vikiwekwa mbalimbali, ukweli utakuwa pamoja na ushujaa, na woga utakuwa pamoja na uwongo.
Ushujaa ni utukufu ung'arao, na woga ni fedheha dhahiri.
Wanyama hujali matumbo yao, na wanyama mwitu hawajali kitu isipokuwa kudhuru wengine.
Wallahi! Mkiukimbia upanga wa maisha ya leo, hamtasalimika na panga za maisha ya Akhera.
Oneni haya kukimbia vitani, kwani huko ni kuvaa deraya ya fedheha na kuingia katika Moto.

(41) Ubora

Ubora wapatikana kwa hamu tukufu za mtu, wala si mafupa yaliyooza ya mababu.
Ubora watokana na akili na adabu, wala hauto­kani na utajiri na nasaba.
Mapenzi ya mababu ni mfungamano kati ya vizazi.
Mwana mwovu huharibu heshima na huwaaibisha mababu zake.
Watu hushabihiana zaidi na marika zao kuliko mababu zao.

(42) Utajiri

Kwa kuvumilia mashaka mali hupatikana.
Madeni mengi humfanya mkweli awe mwongo na avunje ahadi.
Wingi wa mali huharibu nyoyo na huzidisha madhambi.
Mali yako haipotei utumiapo kuhifadhi heshima yako.
Aiasiye dunia itamtii.
Mwenye kujifanyia uchoyo kwa mali yake mwe­nyewe, humlundikia mume wa mke (mjane) wake.
Khiana mbaya kabisa ni khiana katika amana.
Kuchuma mali kwa njia ya halali ni katika mafani­kio ya mtu.
Usimhesabu tajiri yule asiyetumia mali yake kwa wengine.
Dhambi mbaya kabisa ni kula mali ya mayatima.
Takeni kinga ya Mwenyezi Mungu kutokana na ulevi wa utajiri, kwani una ulevi ucheleweao kurejesha fahamu yake.

(43) Ukinaifu

Hakuna utajiri mkubwa kama ukinaifu.
Aridhiaye na aliyopewa na Mwenyezi Mungu hatahuzunika na asiyokuwa nayo.
Mwenye kutosheka na kidogo, hana haja ya nyingi.

(44) Umaskini

Akupendaye hukukataza (mabaya).
Usihuzunike na umaskini na balaa, kwani dhahabu hujaribiwa (husafishwa) kwa moto, na muumini hujaribiwa kwa balaa.
Adhihirishaye umaskini wake, hujidhalilisha nafsi yake.

(45) Tamaa

Mwenye tamaa ni maskini hata akimiliki dunia nzima.
Tamaa humdhalilisha mtu; mauti ni bora kuliko madhila ya kuomba.
Vichwa vya watu huinamishwa kwa tamaa.
Ladha ya mkarimu ni kuwalisha watu; ladha ya mtu duni (bakhili) ni kujilisha mwenyewe.
Bakhili ni hazina kwa warithi wake.
Mtu duni akizidi kuliko kiwango chake, mwendo wake hubadilika.

(46) Takwa Na Uchu

Uchamungu ni ngome madhubuti.
Zaka ya uzuri ni usafi wa moyo.
Akili haiwi pamoja na uchu.
Mwanzo wa matamanio ni furaha, na mwisho wake ni maangamizo.

(47) Afya

Afya ni neema bora kabisa.
Lipa kisasi cha uroho kwa ukinaifu kama vile ulipavyo kisasi kwa adui wako.
Kunyweni maji ya mvua, kwani husafisha mwili na huondoa maradhi.
Dawa yenye kufaa kabisa ni kutotaraji.
Dhana nzuri ni utulivu wa moyo na uzima wa mwili.
Ponesheni maradhi yenu kwa kutoa sadaka.
Vitu viwili havitambuliwi thamani zake mpaka vikosekanapo: ujana na afya.
Afya ya mwili ni uangalifu (katika ulaji).
Awafichiaye madaktari maradhi yake huufanyia hiana mwili wake.
Asiyestahamili maumivu ya kujizuia kula, ataka­wilisha ugonjwa wake.
Jihadhari na ulafi, kwani alaye sana huzidisha maradhi yake na huharibu usingizi wake.
Jua kwamba utajiri wa mali ni neema, na mwili mzima ni bora kabisa kuliko utajiri wa mali, na moyo safi (takwa) ni bora kuliko mwili mzima.
Utamu wa maisha hupatikana kwa kuwa na afya nzuri.

(48) Kujizuia Na Sadaka

Ulevi wa mghafala na majivuno unakawia kutoka kuliko ulevi wa pombe.
Utajiri wa maskini ni ukinaifu wake; utajiri wa mwenye hekima ni elimu yake.
Ajikaniaye ametajirika.
Mwenye kupunguza kula kwake husafisha fikra yake.
Muumini hali kushiba nduguye akiwa na njaa.
Ukilisha shibisha.

(49) Fursa

Fursa hupita kama mawingu, basi faidika na fursa nzuri.
Fursa iliyoachwa ni muhali kurejea kwake.
Tumia fursa iwezekanapo, kwani ikutokapo hutoipata.
Fursa huondoka upesi, huchelewa kurejea.
Usiku na mchana hukufanyia kazi, hivyo zifanyie kazi; nazo hukutumia, nawe zitumie.
Wakati wako ni sehemu za umri wako, hivyo usipitishe wakati wako katika jambo lisilokufaa.

(50) Subira

Dahari ni siku mbili: siku moja pamoja nawe, na siku nyingine dhidi yako; ikiwa pamoja nawe usiringe, na ikiwa dhidi yako subiri.
Pupa hulaumiwa katika kila jambo isipokuwa katika kukabiliana na ubaya.
Mara ngapi umepata mema kutoka mahali usipotazamia!
Nakuusia usubiri wakati wa dhiki na balaa.
Agongaye mlango daima atafunguliwa.
Avumiliaye atashinda.
Mwenye kusubiri hutuliza misiba yake.
Uchungu wa kusubiri hutoa matunda ya ufanisi.
Subirini faraja wala msikate tamaa katika rehema ya Mwenyezi Mungu.
Hakika mashaka yana vikomo, na vikomo vina mwisho, basi subirini mpaka mwisho ufike.
Ikiwa huwezi kuwa mvumilivu, jidai kuvumilia, kwani ni muhali mtu ajishabihishe na watu bila ya kuwa kama wao.

(51) Msamaha

Msamaha (afu) ni uzuri wa nguvu.
Msamaha ni taji Ia mema.
Mtie adabu mtumishi wako amwasipo Mwenyezi Mungu, lakini msamehe akuasipo wewe.
Kubali udhuru wa mwenye kukuomba msamaha.
Ukimshinda adui wako, fanya kumsamehe kwako kuwa ni shukrani (yako kwa Mwenyezi Mungu).
Mtu mbaya kabisa ni yule asiyekubali udhuru na asiyesamehe kosa.
Akiriaye kosa lake huvumilia kosa la mwingine.
Usifanye haraka katika kumwadhibu mtu kuto­kana na kosa (alilolifanya), bali toa nafasi ya msamaha baina ya vitendo viwili hivyo.
Lililo bora kuliko kuomba msamaha ni kuacha kufanya dhambi.

(52) Huruma

Kuwa mpole kwa wanyama; usiwatendee vibaya wala usiwatwishe mizigo kuliko uwezo wao.
Awahurumiaye mayatima atahurumiwa watoto wake.
Asiye na huruma kwa wengine hatoonewa huruma.

(53) Ahadi

Mwungwana akiahidi hutimiza, na akiwa na nguvu husamehe.
Ahadi ni mkopo na mema ni malipo yake.
Ahadi ya muungwana ni fedha (na dhahabu).
Usitoe ahadi kwa jambo usiloweza kulitimiza.
Kukataa kwa uzuri ni bora kuliko kuchelewesha ahadi.

(54) Hamaki

Hamaki ni moto uliokokwa; aipozaye (hamaki yake) huuzima (moto), na aipandishaye hujiunguza.
Dhibiti kinga ya nafsi yako na ukali wa ghadhabu yako mpaka ghadhabu yako ipoe na akili yako irejee.
Jihadhari na hamaki, kwani mwanzo wake ni wazimu na mwisho wake ni majuto.
Mtu bora kabisa ni yule avunjaye ghadhabu yake, na atiaye maanani nguvu zake.
Ukali ni aina moja ya wazimu, kwa kuwa mwenye kuwa nao hujuta, na asipojuta wazimu wake huzidi.

(55) Adabu

Unyenyekevu humtukuza mtu; takaburi humdha­lilisha.
Watu huingiliana kwa kutumia upole.
Mirathi bora kabisa ya wazee kwa wanao ni adabu.
Ingilianeni na watu kwa uzuri kwa kadiri kwamba mkifa wakulilieni, na msipokuwepo machoni mwao waku­tamanini.
Sikilizana na watu ufaidike na mapenzi yao, na kutana nao kwa uso wa bashasha uondoe uhasama wao.
Endeana vizuri na adui wako, na kuwa na moyo safi kwa rafiki yako ili uhifadhi urafiki na upate uungwana.
Kila kitu huhitajia akili, na akili huhitajia adabu.
Mwenye kukosa adabu, utukufu wa nasaba yake hauwezi kumtukuza.
Hakuna vazi bora kuliko adabu.

(56) Kujidhibiti

Mheshimu akufundishaye elimu na uwafundishao.
Jihadhari na kuwaashiki sana wanawake na ku­shawishika kwa raha, kwani kuashiki sana ni matatizo na kupenda sana raha ni udhaifu.
Mwenye nguvu kabisa ni yule ayashindaye mata­manio kwa elimu yake.
Azidishaye matamanio yake hupunguza akili yake.
Yule ambaye matamanio yake huishinda akili yake hufedheheka.
Apendaye kufikia daraja za juu, ayashinde mata­manio yake kwanza.
Hauthaminiki utamu wa raha mbele ya uchungu wa taabu.
Mwenye nguvu kuliko wote ni yule mwenye kuwa na nguvu juu ya nafsi yake.

(57) Uhasidi

Uhasidi huyeyusha mwili.
Bakhili yu dhalili daima; hasidi yu mgonjwa daima.
Uhasidi ni kifungo cha roho.
Uhasidi ni ugonjwa usiopona ila kwa kuangamia hasidi au kwa kufa mhusudiwa.
Rafiki mbaya kabisa ni hasidi.
Sababu ya huzuni ni uhasidi.
Hamu duni ni kumwonea wivu rafiki kwa ufanisi wake.

(58) Ugomvi Na Hitilafu

Ugomvi ni dalili ya maangamizo.
Fitna huzaa huzuni.
Mambo yaliyopangwa vizuri huharibiwa na hitilafu.

(59) Shukrani

Mshukuru akufanyiaye hisani, na mfanyie hisani akushukuruye.
Mwendekeze sana yule uliyemzidi kwa ubora, kwani hii ni aina moja ya kushukuru.
Tambueni haki za yule atambuaye haki zenu, awe mdogo au mkubwa, mnyonge au mtukufu.

(60) Mwendo Murua

lktisadi ni nusu ya matumizi.
Mwenye busara haahirishi kazi ya leo hadi kesho.
Jihadhari na kila kitendo ambacho ukiulizwa aliyekitenda utaona haya na utakikataa.
Jihadhari na kila jambo ambalo likidhihirika litamwadhiri na kumdhalilisha aliyelifanya.
Kwa kuzingatia matokeo utajidhamini na maanga­mizo.
Matokeo ya haraka ni kujikwaa.
Mambo bora kabisa ni ya wastani wake.
Jihadhari na njia uiogopayo kupotea kwake.
Mpanda farasi mwenye matata hujitafutia balaa.
Nashangazwa na mtu azungumzialo jambo ambalo likisimuliwa litamdhuru, na lisiposimuliwa hanufaiki nalo.
Farasi wa mbio hujikwaa pia.
Mwenye haraka huteleza.
Mwenye kuhangaika kutafuta maji katika sarabi, huzidisha taabu yake na kiu yake.
Amchimbiaye kisima nduguye, huingia mwe­nyewe.
Awafanyiaye watu uadui, hujitafutia majuto.
Mwenye kujitia mwenyewe katika taabu kwa jambo lisilomfaa, hujitafutia jambo litakalomdhuru.
Mwenye kukwepa njia safi, hujitumbukiza shi­moni.
Ampandaye farasi mbovu atapotezwa na farasi wake.
Mwenye kuingiliana na kundi la waovu, atatuhu­miwa.
Jihadhari usalimike.
Mwenye kutazama matokeo (ya amali), atasali­mika na balaa.
Mwerevu yu macho; mghafilifu amelala.
Unyofu mkubwa kabisa ni kutopanga jambo katika siri ambalo utalionea haya litakapodhihirika.
Kutamani kwingi anasa humpoteza na humharibu mtu.
Usiufunge mlango utakaokushinda kuufungua.
Usihadithie jambo uliogopalo litakadhibishwa.
Usipigane dhidi ya yule usiyeweza kujitetea.
Usikazane kukaa mahali pa wakubwa katika mjumuiko.
Usifurahie kuanguka kwa mwenzako, kwani wewe hujui litakalokufika siku moja.
Usimshirikishe mtu mwoga katika uamuzi wako, kwani atakudhoofisha katika (kuamua) jambo, na atalitu­kuza lisilokuwa kubwa.
Usiingiliane na mfalme wakati anapokuwa na msukosuko; kwani ikiwa bahari haiwezi kuwa salama kwa mpanda chombo licha ya ushwari wake, basi vipi isiweze kumwangamiza kwa pepo zake zivumazo na mawimbi yake makali?
Usiache moyo wako uone huzuni kwa yale yaliyo­pita, kwani yatakushughulisha usijitayarishe kwa yale yatakayokuja.
Jihadhari na kudhihirisha uasherati, kwani huko ni kutenda dhambi mbaya zaidi.
Jihadhari na kuchanganyika na waovu, kwani wao ni kama moto, huwaunguza wausogeleao.
Mtii aliye juu yako, utatiiwa na aliye chini yako.
Jihadhari na kuingiliana na wenye kutoa aibu za watu, kwani hakuna atakayesalimika (na kuumbuliwa) atakayesuhubiana nao.
Jihadhari na kufanya urafiki na watu mafasiki, kwani mwenye kuridhika na vitendo vyao, huwa ni mmoja wao pia.
Ukiona kwa mwenzako tabia isiyopendeza, basi jiepushe mfano wake usitokeze kwako.

(61) Toba

Kutubu hufuta dhambi.
Ujitengapo na dhambi (baada ya kutenda), tubu.
Aachaye dhambi huwa amerejea (kwa Mola wake).

(62) Kutakasa Nafsi

Wapendelee watu yale uyapendeleayo mwenyewe.
Fanya nafsi yako kuwa ni kipimo baina yako na mwingine; ukipendacho mpendelee mwenzako pia, na uki­chukiacho usimtakie mwenzako pia. Mfanyie mema kama vile upendavyo akufanyie wewe, na wala usidhulumu kama vile hupendi kudhulumiwa.
Iheshimu nafsi yako kutokana na kila uduni hata ikiwa ni kujitia katika hatari, kwani hutaweza kupata kitu kingine badala ya heshima ya nafsi yako.
Aondoshaye chuki hutuliza moyo na mawazo yake.
Jitakase nafsi yako kutokana na kila uduni hata kama itakuvutia kwenye uyapendayo.

(63) Kisasi

Kitendo kibaya kabisa cha mwenye nguvu ni kuchukua kisasi.

(64) Maadili

Kujiweka mbali na maovu ni bora zaidi kuliko kutafuta mema.

(65) Kushuku

Kumshuku mtu mwema ni dhambi mbaya kabisa na dhuluma mbaya sana.
Ondosheni dhana mbaya kati yenu.

(66) Majaaliwa

Ikiwa majaaliwa hayageuki, basi uangalifu hauna maana.
Hii ngozi nyembamba haiwezi kuvumilia moto wa Jahannam.

(67) Hiana

Amfanyiaye hiana mtawala wake hupoteza usa­lama wake.
Mwenye kumfanyia hiana waziri (msaidizi) wake huharibikiwa uendeshaji wake.

(68) Uvivu

Mwenye kupoteza wakati wake atajuta.
Ulegevu husababisha uvivu.

(69) Upotevu

Vipi mtu amwongoze mwingine ikiwa mwenyewe amepotea?

(70) Anuwai

Ada ni tabia ya pili.
Mwenye kufikia kilele cha akipendacho, basi atazamie kilele cha akichukiacho.
Aliyechafua asili yake amechafua wajihi wake.
Aombaye zaidi ya kiasi chake, astahiki kunyimwa.
Aingilianaye na wapumbavu hudharauliwa.
Wanyama hujali matumbo yao, na wanyama mwitu hawajali kitu isipokuwa kudhuru wengine.
Si kila alengaye hupata shabaha.
Kudanganyika na wanawake ni tabia ya kipu­mbavu.
Tumaini ni kama sarabi, humdanganya aionaye, na humvunja moyo aitumainiaye.
Hiana hurudufu maovu.
Alipoulizwa kuhusu masafa baina ya mashariki na magharibi. Imam Ali (amani iwe juu yake) akajibu: "Ni msafara wa jua katika siku moja."