read

Hii ni Surah Abasa

Sura Abasa 80

Imeteremshwa Makka, ina Aya 42.

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

1. Yeye aliukunja uso akapa mgongo. 1

2. Kwa sababu alijiwa na kipofu. 2

3. Ni lipi kilichokufanya wewe kujua kuwa yeye atajitakasisha,

4. Au akawaidhika ukamfaa waadhi ?

5. Ama kwa yule ajifikiriaye kuwa amejitosheleza (katika utajiri wa mali yake),

6. Na kwa huyo anamshughulikia,

7. Wala haitakuwa lawama juu yako iwapo hatajitakasa.

8. Ama yule anayekuijia kwa jitihada na moyo mnyenyekevu,

9. Na akiwa na khofu (moyoni mwake),

10. Wewe kwake huyo utamshughulikia na kumsikia

11. Sivyo ! Hakika (Quran) hii ni nasaha. 3

12. Basi kila apendaye atawaidhika,

13. (Yameandikwa hayo) Katika Vitabu vilivyohishimiwa.

14. Vilivyotukuzwa, vilivyotakaswa,

15. Vilivyo katika mikono ya wajumbe Malaika

16. Watukufu, watiifu wa Mwenyezi Mungu.

17. Amelaaniwa Mwanadamu ! Namna gani alivyokuwa bila shukrani ?

18. Kwa kitu gani Amemuumba ?

19. Kwa tone la manii, alimuumba, kisha akamwekea vipimo vyake.

20. Kisha akafanyia njia nyepesi.

21. Kisha akamfisha na kumfanya azikwe kaburini.

22. Kisha aendapo atamfufua.

23. La ! Hakutimiza vile alivyokuwa ameamrishwa.

24. Basi mtu na akitazama chakula chake. 4

25. Kuwa ndio sisi tuliomiminisha maji, mmiminiko wa nguvu

26. Kisha tukaipasua ardhi, kwa mipasuko (iliyo lazima),

27. Na tukafanya sisi kuota nafaka humo

28. Na Zabibu na mboga

29. Na Zaituni na Mitende

30. Na mabustani yenye miti mingi

31. Na matunda na malisho

32. Kwa manufaa yenu na wanyama wenu.

33. Basi itakapo kuja sauti kali iumizayo masikio (Sauti ya baragumu la kiyama)

34.. Siku ambayo mtu atakimbia ndugu yake.

35. Na mama yake na baba yake

36. Na mke wake na watoto wake

37. Kila mtu katika wao, siku hiyo atakuwa na jambo la kumshughulisha.

38. (Kutakuwepo) nyuso zing’aazo siku hiyo,

39. Zitacheka na kufurahika 5

40. Na (Zitakuwapo) nyuso katika siku hiyo zenye vumbi,

41. Kiza kitakuwa kimevikwa juu ya nyuso zao. 6

42. Hao ndio makafiri, waliokuwa wakitenda maovu

 • 1. Chanzo cha kuteremshwa kwa Sura hii ni tukio la kihistoria. Wakati mmoja, Mtume s.a.w.w. alikuwa amekaa pamoja na wakuu wa kabila la Qureish ndipo hapo alipofika Sahaba Abdullah ibni Maktum ambaye alikuwa kipofu. Hapo Mtume s.a.w.w. alimpokea kwa furaha na heshima na alimkalisha karibu naye. Kwa kuwa Abudullah alikuwa ni mtu maskini na ni kipofu, wakuu wa Qureish walimtazama kwa dharau na hawakufurahishwa kwa heshima na nafasi aliyopatiwa mbele yao, na hapo ndipo mmoja wao alipoufinya uso wake na kumpa mgongo. Tendo hili halikumpendeza Allah s.w.t. na Jibraili aliiteremsha Surah hii papo hapo. Ni jambo la kusikitisha mno kuona kuwa baadhi ya Mufassiriina ili kutaka kumlinganisha Mtume s.a.w.w. sawa na watu wengineo, wamethubutu hata kusema kuwa alikuwa na kasoro za adabu kwani alimdhalilisha Abdullah, wakati ambapo aliyemdharau ni miongoni mwa Sahaba. Ni wazi kabisa kupuuzwa kwa tukio la kihistoria na pili ni masingizio juu ya Mtume s.a.w.w. ambaye ni bora wa maadili, Kiigizo kwa wanadamu wote. Ni ukweli usioshukiwa wa kihistori kuwa Islam haikuenezwa kwa makali ya upanga bali kwa maadili ya Mtume s.a.w.w. na tabia yake iliyokuwa njema kabisa miongoni mwa watu wote. Ukweli ni kwamba, upanga uliotumiwa na Islam ulikuwa ni kwa ajili ya kujihami tu na kuwahifadhi Waislam wake wa hapo mwanzoni dhidi ya uchokozi wa maadui wake

  Kwa kukubali kuwa Mtume s.a.w.w. alikuwa na kasoro, basi ni kupinga na kukana Aya za Quran, 68:4 “Na kwa hakika wewe umesimama kabisa katika tabia njema” (vile vile tazama 2:143,33:45, 33:21). Je itawezekanaje kukubali kwetu kwa uzushi huo wa kasoro wakati ambapo Allah swt anawaamrisha wanadamu wote kufuata mfano wa Mtume s.a.w.w. katika tabia na maadili ?
  33:21 “Kwa hakika (kwake) ni kwa ajili yenu katika Mtume wa Allah (Muhammad) Mfano bora kabisa (tabia na maadili) kwa ajili ya yule aliye na matumaini ya Allah na siku ya baadaye (Kiyama) na kumkumbuka mno Mwenyezi Mungu”

  Kosa kubwa ni kule kutokutumia na kutokuielewa lugha vile vile ilivyotumika na vile vile kutozitilia maanani riwaya na tafsiri zilizotolewa na Ahli Bayt a.s. ya Mtume Mtukufu s.a.w.w.

 • 2. Anayeambiwa ni Mtume s.a.w.w. lakini ina maanisha kwa Sahaba.
 • 3. Mafundisho ya Quran ni kwa ajili ya wote na wala mtu asikatazwe kwa sababu ya umaskini wake au udhoofu alionao, bali ucha Mungu uwe kipaumble.
 • 4. Mtu anakumbushwa juu ya neema za Allah, zilizoteremshiwa juu yake, kwa hiyo ndiyo uhai wake na viumbe vyote. Vile vile rejea 79:33.
 • 5. Hii itakuwa ni katika hali ya furaha na mafanikio kwa ajili ya waumini na wale waliookoka.
 • 6. Hii ina waelezea wale hali yao itakavyo kuwa ya makafiri na watenda maovu na yatakayokuwa yamewapata.